Habari za Punde

Mgongano kisera wakwamisha vita dhidi ya HIV


Na Ali Haji, Pemba
WADAU wa mapambano dhidi ya UKIMWI Zanzibar wamelalamikia tatizo la mgongano wa sera zinazosimamia mapambano hayo kuwa zinakwamisha kupatikana kwa mafanikio endelevu.

Wadau hao walitoa malalamiko hayo hoteli ya Visitors Inn Jambiani katika warsha ya kutengeneza ujumbe wa kuisaidia jamii kubadilisha tabia hatarishi zinazopelekea maambukizo ya VVU na UKIMWI.

Akitoa mfano Sihaba Saadat, Afisa Elimu na Uraghibishaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC), alisema wakati sera ya Ukimwi ikielekeza kwamba kila mwananchi ni lazima ahakikishiwe upatikanaji wa huduma za kinga na matibabu ya VVU na UKIMWI, sera nyengine inayohusiana na utumiaji wa dawa za kulevya inakataza watumiaji wa dawa kumilikishwa mabomba ya sindano ambayo wangeyatumia kwa usalama zaidi na kuepuka kuchangia bomba moja la sindano kwa watu wengi na kusababisha maambukizi miongoni mwao.

Alisema wakati nchi nyingi zikiwemo Mauritius zikiwa zimepata mafanikio ya kupunguza kasi ya maambukizi ya VVU kupitia mpango wa kutoa mabomba ya sindano yaliyo salama kwa watumiaji wa dawa wanaojidunga sindano, bado sera za Zanzibar zinapingana kuhusu hilo, jambo ambalo limepelekea kundi la watumiaji wa dawa za kulevya wanojidunga sindano kuwa na kiwango kikubwa cha maabukizi.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni bado makundi maalum ndiyo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi kulinganisha na jamii ya kawaida ambapo takwimu zinaonesha wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano wana asilimia 16 ya maambukizi, wanaume wanafanya mapenzi ya jinsia moja aslimia 12.8 na wanawake wanaokodisha miili yao wana kiwango cha maambukizi cha asilimia 10.8

Nae Zeud Nassor alisema pamoja na mgongano wa sera kumekuwepo pia na tatizo la misimamo mikali ya viongozi wa taasisi za kiserikali na za kidini juu ya njia za kupunguza maambukizi kwa makundi maalum huku wakiyaona makundi hayo kama vile si sehemu ya jamii.

Alisema hali hiyo inapelekea makundi hayo kujiona kuwa yametengwa hali inayoongeza tatizo la unyanyapaa.

Naye Ahmed Abdulrahman alisema imefika wakati sasa kwa wadau walio katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, kusaidia mabadiliko ya kisera yatakayohakikisha huduma za kinga, tiba na matibabu kwa watu wote yakiwemo makundi maalum ambayo ni sehemu pia ya jamii ya Wazanzibari.

Tafiti za kitengo cha kudhibiti maambukizi ya UKIMWI Zanzibar (ZACP) zinaonesha kuwa kumekuwepo na maingiliano makubwa kati ya makundi ya watumiaji wa dawa za kulevya, wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, wanawake wanaokodisha miili yao na jamii ya kawaida jambo ambalo limeweka daraja ya uwezekano wa maambukizi kuvuka kutoka sehemu moja kwenda nyengine ya jamii kwa urahisi.

Katika warsha hiyo wadau hao walijikita zaidi katika kutengeneza vipeperushi, mabango na vijumbe vyenye mwelekeo wa kubadili tabia hasa zile zinazohusiana na unyanyasaji wa kijinsia, uangalizi wa wagonjwa majumbani, unyanyapaa na utafutaji wa huduma za kinga na tiba zinazoendana na UKIMWI.

Pia mkazo katika mkutano huo ulitolewa kuandaa ujumbe maalum utakaofikia makundi yaliyo katika hatari zaidi aidha ya kuambukiza ama kuambukizwa VVU.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.