Na Mwashamba Juma
TAASISI za usafirishaji na uingizaji mizigo katika nchi za Afrika Mashariki zimetakiwa kujipanga kibiashara ili kukabiliana na changamoto za kimataifa wanazokabiliana nazo katika utendaji wao wa kazi.
Aidha aliwataka kuzijua sera na sheria za kimataifa ili kuepukana na gharama wakati wa uingizaji na usafirishaji lengo la kuepuka gharama kubwa.
Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Thuwaiba Edington Kisasi alitoa nasaha hizo alipofungua mafunzo ya siku tatu kwa taasisi hizo kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maeneo jirani katika hoteli ya Blue bay Kiwengwa, mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaweka pamoja na kuelezana changamoto wanazopambana nazo kila siku ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Aliwataka wadau hao kufuatilia kwa makini mafunzo yatakayotolewa na kubadilishana uzoefu pamoja na kujadili changamoto wanazopambana nazo na kuzipatia ufumbuzi.
Hata hivyo aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kutembelea sehemu muhimu za Zanzibar ikiwemo vivutio muhimu vya utalii na sehemu za Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Kwa upande wao washiriki,walisema mbali na kubadilishana uzoefu pia mafunzo hayo yatawatambulisha na kuwakutanisha katika kuweka mtandao mzuri wa biashara jambo ambalo litakuza mahusiano mema na kuimarisha ujirani mwema.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Jumuiya inayojishughulisha na masuala ya usafirishaji na uingizaji wa mizigo kwa nchi zote za Afrika Mashariki ya East Coast, Kenneth Mwige kutoka Kenya, alisema lengo la jumuiya hiyo ni kuwasaidia wafanyabiashara wa Afrika Mashariki kupunguza gharama za kufanya biashara ndani na nje ya mipaka ya nchi zao.
Aliongeza kuwa changamoto kubwa wanazopambana nazo ni pamoja na kulipia gharama za usafirishaji katika nchi za kigeni zikiwemo bima na ushuru mwengine.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Usafirishaji Mizigo Zanzibar, Abdul-Wahid Talib Ali alisema Zanzibar ni kituo kilicho karibu katika nchi zote za Afrika Mashariki lakini kinaongoza kwa kutoza gharama kubwa wakati wa uingizaji na usafirishaji mizigo.
Mafunzo hayo yamezishirikisha nchi za Afrika Mashariki, Sudan Kusini na Zambia.
No comments:
Post a Comment