Habari za Punde

Uzinduzi umeme mpya Unguja kesho

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za uzinduzi wa umeme mpya Zanzibar kesho katika uwanja wa Amaan.
 
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdalla Shaaban, alisema sherehe hizo zitanza saa nne asubuhi, ambapo Dk. Shein ataanza kuzindua kituo cha kusambazia umeme kilichopo Mtoni.
 
Alisema sherehe hizo zitahudhuriwa na viongozi mbali mbali wa chama na Serikali hivyo amewataka wananchi kutoka maeneo mbali mbali, kufika kwa wingi katika viwanja hivyo, ili kuweza kufahamu mambo mengi yanayohusu mradi huo.


Akitoa muhtasari wa mradi, Waziri Shaaban alisema tangu mwaka 2008 serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilianza harakati za kutafuta umeme wa uhakika baada ya kuona kuwa umeme uliopo hivi sasa haukidhi haja ya matumizi kwa wananchi wote wa kisiwa cha Unguja.
 
Alisema kwa muda huo wa miaka mitano mwaka 2012 walifanikiwa kuanza ujenzi wa mradi huo kupitia ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia mradi wa MCC, ambao umegharimu dola za Marekani milioni 68, ambapo serikali ya Zanzibar imechangia dola milioni 1.4 ambazo zimetumika katika kulipia fidia za mali mbali mbali za wananchi zilizoathirika kwa kupitisha umeme huo.

Alisema waya huo una uwezo wa megawati 100 ikilinganishwa na waya wa zamani ambao ulikuwa na uwezo wa megawati 40, ambapo matumizi ya umeme kwa wananchi wa Unguja ni megawati 50 hadi 55.

Kuhusu kukatika umeme mara kwa mara,alisema hali hiyo inatokana na sababu nyingi na kwamba tatizo hilo litaendelea huku shirika la Umeme Zanzibar likiendelea na jitihadi za kuzirekebisha.

1 comment:

  1. Sasa huu umeme utapatikana au kama siku zote tulivyozoea kukatika katika! maaana hapa sijamuelewa muheshimiwa

    "Kuhusu kukatika umeme mara kwa mara,alisema hali hiyo inatokana na sababu nyingi na kwamba tatizo hilo litaendelea huku shirika la Umeme Zanzibar likiendelea na jitihadi za kuzirekebisha"

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.