Habari za Punde

Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano yataja vipaumbele vyake

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

WIZARA ya Miundombinu na Mawasiliano, imeeleza kuwa Mpango wa utekelezaji wa Malengo yake kwa kazi za kawaidia na maendeleo kwa mwaka 2012/13, umeweka vipaumbele kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya Barabara, viwanja vya ndege, bandari pamoja na uimarishaji wa huduma za usafiri na Mawasiliano.


Uongozi wa Wizara hiyo ulieleza hayo katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa mpango kazi kwa kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013.


Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein pia, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.


Uongozi huo, chini ya Waziri wake Mhe. Rashid Seif Suleiman akitoa muktasari wa mpango kazi wa Wizara hiyo alisema kuwa utekelezaji wa vipaumbele hivyo unaendana na utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZAII 2010-2015) ambayo piam ymezingatia Dira ya Maendeleo ya Karne ya 2020.
Waziri Rashid alisema kuwa katika kipindi kilichoanzia Julai 2012 hadi Machi 2013 Wizara ilipanga kutekeleza miradi 14 ya maendeleo ikihusisha miradi ya ujenzi wa barabara, ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege na mradi wa Mageuzi ya mfumo wa taasisi.

Aidha, Wizara hiyo ilieleza kuwa katika kukamilisha ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, hatua za uendelezaji wa ujenzi huo zinaendelea.

Uongoxi huo ulieleza kuwa Wizara imeshatiliana saini na Mshauri wa kufanya mapitio ya usanifu na michoro ya jengo hilo tarehe 29 Machi na Mshauri huyo ataanza kazi rasmi Aprili 17, mwaka huu.
Uongozi huo pia, ulieleza kuwa ujenzi wa barabara ya Mgagadu-Kiwani wenye jumla ya km 6.6 zimekamilika kwa tabaka la pili la kifusi na kueleza kuwa tathmini ya malipo ya fidia ya mali za wananchi wa Kiwani Pemba pamoja na wananchi wengine walioathirika na ujenzi wa barabara imeshafanyika.

Aidha, zoezi la kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhumu wa kununua tiketi kutoka kwa kampuni za usafirishaji wa abiria linaendelea kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na kuwatumia wafanyakazi wa kitengo cha usalama kuwazuia abiria wanaonunua tiketi bila vitambulishi kutosafiri.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi kwa uongozi wa Wizara hiyo juhudi kubwa iliyoifanya katika Mpango kazi wake.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa mafanikio makubwa yaweza kupatikana katika Wizara hiyo huku akisisitiza haja ya kukiimarisha zaidi Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani cha Wizara hiyo kwa kupewa uwezo ili kiendelee kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa ya kuendelea kupata mafanikio Wizara hiyo huku akipongeza kwa jinsi yautekelezaji wa maagizo aliyoyatoa katika vikao vilivyopita walivyoyafanyia kazi.

Dk. Shein alisisitiza kutolewa elimu kwa wananchi juu ya namna bora ya uingiaji wa bandarini kwa wale wanaosafiri na wanaowashindikiza jamaa zao ili kuepuka athari zinazoweza kutokezea katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.