Habari za Punde

Sadifa: Sijawahi kuwa kichaa

Na Shehe Semtawa
 
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Khamis Sadifa Juma, amesema kuwa hajawahi kuugua ugonjwa wa akili (kichaa) kama anavyozushiwa na wapinzani wake.
Alisema kuna watu wameandaliwa na mafisadi ili wamchafue, ikiwezekana aachie ngazi kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Yusuf Hamad Masauni.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu mwishoni mwa wiki, Sadifa alisema wapo baadhi ya watu wamekuwa wakifanya vurugu hizo kwa ajili ya kutaka kujipatia umaarufu kupitia mgogoro huo na kuwafurahisha wale wanaowafadhili kifedha.
Alisema miongoni mwa uchafu aliowahi kutupiwa na watu hao ni kuwa alighushi umri ili aweze kugombea nafasi hiyo.

“Najua nimewekwa kwenye kundi la Edward Lowassa na huyo wamemtaja tangu nagombea, ndiyo maana wananipiga vita kutoka mwanzo.
“Wamegonga ukuta, hao wanatapatapa tu ndugu yangu, hao si wanasiasa ni wana si hasa, watatulia wenyewe, mimi sina muda wa kujibizana na mtu magazetini,” alisema.
Akizungumzia tuhuma hizo, Sadifa, alisema kuwa yeye alizaliwa mwaka 1982 na hivi karibuni ametimiza miaka 31, kwamba ambaye haamini anaweza kujiridhisha kwa kuingia kweye mtandao ataziona taarifa zake zote.
Kuhusu ugonjwa wa kichaa, alisema hizo ni taarifa za kitabibu, hivyo ni vema kwa wale wote wanaodai hivyo kuonesha ushahidi wa vyeti vya madaktari ambavyo vinathibitisha madai yao.
“Mimi ni mbunge sasa kama kuna mtu ananituhumu hivyo basi waende mahakamani kama alivyofanya Raila Odinga kwenda kupinga ushindi wa Uhuru na hatimaye haki ikapatikana,” alisema.
Naye mmoja wa vijana wanaotuhumiwa kutaka kumwondoa madarakani mwenyekiti huyo alisema: “Wakati umefika Sadifa ni lazima aondoke.”
Alisema ataondoka si kwa kuwa wana timu au mkakati uliosukwa wa kumwondoa bali suala la msingi hapo ni kanuni.
“Mimi ni mjumbe wa UVCCM najua kanuni zetu. Sadifa ataondoka si kwa kuwa hatumtaki, hatuutaki uwezo wake mdogo na kanuni alizovunja,” alisema.
Alisema kuwa Sadifa ni mbunge tangu 2010 lakini akahoji ni wapi aliwahi kusikika akizungumzia hoja ya vijana kama vile ajira hata baada ya kuchaguliwa UVCCM?
“Wapi Sadifa amefanya mkutano na kuvutia vijana wajiunge na CCM? Huwezi kumlinganisha hata na John Heche, Mwenyekiti wa BAVICHA wa CHADEMA. Unategemea atasaidia chama, huyu ana uwezo mdogo,” alisema kijana huyo.
 
Chanzo - Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.