Habari za Punde

Denmark kupiga jeki sekta ya afya

Na Fatma Kassim, Maelezo
 
DENMARK imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Zanzibar katika kimarisha sekta ya afya.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Emma Hjernue alisema mbali na Denmark kubadilisha mfumo wa utoaji wa misaada yake kwa Tanzania itahakikisha inalenga kuisaidia zaidi Zanzibar katika kukuza utoaji wa huduma katika sekta hiyo.

Alitoa ahadi hiyo jana wakati akizungumza na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni Haji, ofisini kwake Mnazimmoja.

Alisema Denmark inathmini juhudi za Zanzibar na inalenga kusaidia katika bajeti ya sekta hiyo ila ni vyema kuangalia njia sahihi za utekelezaji wa mpango huo kutokana na kuwepo tofauti za mfumo wa usimamizi wa sekta ya afya kwa Zanzibar na Tanzania Bara.


Alisema Denmark itaendeleza misaada yake kwa Zanzibar kwa vile imekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika nyanja mbalimbali.

Kwa upande wake Waziri Duni alisema bado ufinyu wa bajeti kutoka serikalini unakwamisha juhudi za kuendesha sekta hiyo, hivyo misaada ya wahisani itasaidia kuimarisha huduma hiyo.

Hata hivyo, alisema wizara imeiomba serikali kuu kuongeza bajeti ya sekta ya afya ili kupata fedha za kutosha za kununulia dawa.

Ameishukuru Denmarak kwa misaada wanayoitoa kwa Zanzibar ambayo imesaidia kukuza utoaji huduma za afya.

1 comment:

  1. Inasikitisha sana kwani Denmark ilikuwa ni miongoni mwa nchi zilizokuwa zikisaidia zanzibar sana katika miaka mingi mpaka kufikia miaka ya 80 na mwanzoni mwa 90 sijuwi nini kimetokea hadi kufikia baina yetu na wao wa swedish hawakuwa wapenzi wa zati kwa wazaznibari kama walivyokuwa wa Den leo waswidish ndio wamewapiku denmark unaweza kusema tumepoteza uhusiano wetu na denmark kwa kiasi fulani walikuwa ni watu wenye moyo kwa zanzibar

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.