Habari za Punde

….Hakimu wa Simba, Yanga atajwa. Kiingilio cha chini buku tano, juu 30,000/-

Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
MWAMUZI Martin Saanya kutoka Morogoro, ndiye atakayechezesha pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga la kufunga pazia la ligi kuu ya soka Tanzania Bara Jumamosi wiki hii kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka nchini ili kujionea nani zaidi baina ya miamba hiyo, Saanya atasaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha na Jesse Erasmo kutoka Morogoro, wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.
Kamisaa wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathmini wa waamuzi atakuwa ni Leslie Liunda wa Dar es Salaam.

Aidha Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura, amesema kiingilio cha chini katika mpambano huo, kimepangwa wa shilingi elfu tano, kwa majukwaa yenye viti vya rangi ya bluu.

Amefahamisha kuwa, katika mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni, viingilio vyengine vitakuwa shilingi elfu saba kwa viti vya rangi ya kijani na elfu kumi viti vya rangi ya chungwa.


Kwa upande wa jukwaa La VIP A, bei ya tiketi itakuwa shilingi 30,000, wakati VIP B shilingi 20,000 na wa mashabiki watakaopenda kukaa jukwaa la VIP C watalazimika kulipa shilingi 15,000.


Wambura amesema kuwa, viingilio hivyo ni sawa na vya mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo baina ya miamba hao, uliochezwa Oktoba 3, mwaka jana, na kuishia kwa sare ya bao 1-1. 


Kwa mujibu wa taarifa hizo za TFF, tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa Ijumaa wiki hii katika vituo mbalimbali vitakavyotajwa baadae.


Tayari miamba hiyo ya soka nchini iko mafichoni kwa maandalizi ya mpambano huo, Yanga ikiwa imepiga kambi kisiwani Pemba wakifanya mazoezi uwanja wa Gombani, huku Simba wakijichimbia mjini Zanzibar katika mtaa wa Mbweni nje kidogo ya manispaa hiyo.

Wekundu hao wanafanya mazoezi kwenye uwanja wa Mao Dze Tung kufuatia kufungwa wa uwanja wa Chuo cha Elimu Chukwani, kwa ajili ya matengenezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.