Habari za Punde

New Generation yaamsha soka la wanawake Pemba

Na Abdi Suleiman, Pemba
KUFUATIA ziara ya timu ya soka la wanawake New Generation kutoka Unguja, wadau wa mpira wa miguu kisiwani hapa wamefunguka na kusema ipo haja ya kuanzishwa timu kama hiyo kisiwani Pemba ili ishiriki mashindano mbalimbali.

Wadau hao wamesema, wakati umefika kufuta dhana potofu kwamba mpira wa miguu ni mchezo wa wanaume pekee na kuwa wanawake hawapaswi kuucheza.

Wameeleza kuwa, wanawake pia wanaweza kucheza soka kama walivyoonesha wakati wa mechi kadhaa ambazo New Generation ilicheza uwanja wa Gombani, ili kwenda sambamba na ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

“Sisi tumezowea kusema kuwa, mpira wa miguu ni kwa wanaume peke yao, hata sisi wanawake tunaweza kucheza, si wale pale wanawake wenzetu wanacheza”, alisema Asha Nassor (Asha Top) aliyewahi kuwa Katibu wa netiboli Pemba.

Asha Nassor (Ashatop), alisema kuwa, wamefarajika sana na ujio wa timu hiyo, na kuwanahamu ya kutaka timu hiyo, ibakie na iendelee na michezo yake, ili kuweza kuwahamasisha wanawake kisiwani pemba na kuunda timu yao.



Asha alieleza ujio wa New Generation yenye maskani yake mtaa wa Kwahani mjini Unguja, umewafumbua macho wanawake kisiwani hapa, na kuwapa moyo wa kuanzisha timu hiyo.

Akizungumzia sababu zinazorudisha nyuma jitihada za kuendeleza soka la wanawake Pemba, Asha alisema kukosekana kwa walimu wa mpira wa miguu wa kike wa kufundisha, ni tatizo linalochagia hali hiyo.

Kwa upande wake, mchezaji wa New Generation Mwanakhamis Omar, alisema lengo la ziara yao ni kuhamasisha wanawake wenzao kuanzisha timu yao ili waweze kukuza soka la wanawake kisiwani pemba, huku akiwaomba wazazi kuwaruhusu watoto wao kucheza mpira wa miguu, ambao unaweza kuwa ajira itakayowainua kimaisha kama wataendelezwa vyema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.