Na Mwandishi Wetu
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Simba SC umesema hauna imani na mabadiliko ya mwamuzi yaliyofanywa kuelekea mpambano wao na Yanga SC Jumamosi, na kwa sababu hiyo unakutana katika kikao cha dharula haraka iwezekanavyo kujadili suala hilo, ikibidi kususia mchezo huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba inayosimamia ushiriki wa timu katika mashindano, Zacharia Hans Poppe, amekaririwa jana jioni akisema kwamba uongozi utakutana haraka kujadili mabadiliko hayo.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema taarifa rasmi waliyokuwa nayo awali, mwamuzi aliyepangwa kuchezesha mechi hiyo ni Israel Nkongo, lakini ajabu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana limemtaja Martin Saanya.
“Haiwezekani mabadiliko yafanyike ghafla, lazima kutakuwa kuna namna hapa. Tunakutana mara moja kujadili na kuchukua hatua, ikiwezekana tunaweza kugomea hiyo mechi, iwapo tutagundua kuna mchezo mchafu umeandaliwa dhidi yetu”, alisema Hans Poppe.
Saanya kutoka Morogoro ndiye ameteuliwa kuchezesha pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga SC la kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment