Na Mwandishi wetu
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kasim Tindwa, amewataka wananchi wa
kisiwani hapa kuwa wabunifu katika shughuli zao za kila siku, ili kubadilisha
hali ya maisha waliyonayo na kuingia katika ushindani wa kimaendeleo.
Tindwa alitoa kauli hiyo kisiwani Pemba jana wakati akifungua majadiliano ya
ushirikiano kwa manufaa ya wote (smart partnership dialogue) ikiwa ni mwendelezo
wa majadiliano yanayofanyika katika kanda mbalimbali nchini.
“Watu wa kisiwani Pemba lazima tubadilike, tuondoe ule uzamani tulionao,
majadiliano haya yana maana kubwa sana kwetu, ni lazima tuzingatie yale
yatakayozungumzwa na watoa mada ili tukitoka hapa tuwe na mtazamo tofauti,”
alisema Tindwa.
Alisisitiza kutokana na kaulimbiu ya majadiliano haya kuwa ni ‘matumizi ya
teknolojia katika kuleta maendeleo endelevu’, ni lazima watu wabadilike kwa kila
nukta ya kazi zao wanazofanya, waweke ubunifu zaidi ya kukaa na kushikilia yale
ya zamani,” alisema.
Alisema Baraza la Biashara la Zanzibar (ZBC) liko bega kwa bega na Baraza la
Taifa la Biashara (TNBC) katika kuhakikisha majadiliano haya yanaleta tija na
nguvu ya pamoja katika kuleta maendeleo ya wananchi wa Tanzania Bara na Tanzania
Visiwani.
Mkuu wa Fedha na Utawala wa TNBC, Oliva Vegulla, alisifu ushiriki na michango
mbalilimbali kutoka kwa washiriki wote katika mkutano huo.
TNBC ndio waliopewa dhamana ya kuratibu majadiliano hayo ya kikanda na ya
kitaifa pia.
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment