Habari za Punde

Polisi, JKU zaua ligi ya kikapu. Al Yussuf/Thabit Kombo Cup’ Pemba kuanza leo

 MICHUANO ya ligi ya mpira wa kikapu kanda ya Unguja, imeendelea juzi katika uwanja wa Maisara huku maafande wa Polisi wakiichezesha kwata timu ya Beit el Ras kwa kuimiminia vikapu 84-31.

Kwa ushindi huo, Polisi imefikisha pointi kumi sawa na Rangers ambao wanatarajiwa kukutana nao leo.
Katika mchezo huo Polisi, ilionekana kucheza wa kiwango kizuri tafauti na
hapo awali, na kuweza kufanya vizuri katika robo zote nne.

Na katika mchezo mwengine wa ligi hiyo, wajenga uchumi wa JKU, nao wakawadidimiza Spiders kwa ushindi wa vikapu 64-48.
Spiders, ndiyo timu pekee inayoongoza kwa kufungwa vikapu vingi tangu kuanza kwa ligi hiyo.


Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho lwa michezo miwili, ambapo African Magic itaoneshana kazi na Spiders, huku Rangers wakipimana ubavu na maafande wa Polisi.

Katika hatua nyengine, mashindano ya mpira wa kikapu yaliyopewa jina la ‘Al Yussuf/Thabit Kombo Cup’, yanatarajiwa kuzinduliwa leo kisiwani Pemba.

Michuano hiyo itakayoshirikisha timu 13 zikiwemo 11 za wanaume na
mbili za wanawake, itafunguliwa kwa mchezo kati ya mabingwa
watetezi Tornadoes na Mkoani.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, anatarajiwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Ocean Group of Hotels, Amani Ibrahim Makungu aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kabla hajajiuzulu mapema mwaka huu.

Mabingwa katika michuano hiyo kwa wanawake na wanaume, watazawadiwa
shilingi laki tatu, mipira mitatu na jezi seti moja, huku washindi wa pili wataondoka na shilingi laki mbili, mipira miwili na seti moja ya jezi kila timu.

Timu itakayoshika nafasi ya tatu kwa upande wa wanaume pekee, atafutwa jasho kwa zawad ya seti moja ya jezi, mpira mmoja na shilingi laki moja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.