Habari za Punde

Majeruhi wa bomu wafikia 70. Watu kadhaa washikiliwa. Mbunge Chadema apigwa, aumizwa jicho

Na Joseph Ngilisho, Mahmoud Ahmad, Arusha
IDADI ya watu waliojeruhiwa katika shambulizi la bomu lililotokea katika mkutano wa kampeni wa chama cha Chadema mjini Arusha na KCMC mkoani Kilimanjaro.

Majeruhi waliolazwa hospitali ya Seliani ni 40, tisa wanatibiwa hospitali ya mkoa Mount Meru na majeruhi 7 wanatibiwa hospitali ya Saint Elizabert huku hali zao zikiendelea vizuri, isipokuwa wagonjwa wanne ambao hali zao sio nzuri.

Miongoni mwa majeruhi ambao hali zao sio nzuri ni mtoto Farad Jamal (7) ambae yupo kwenye chumba cha uangalizi maalum (ICU) katika hospitali ya KCMC.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea majeruhi hao, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo aliwataja waliofariki kuwa ni Judith William Mushi(46) ambaye alikuwa Katibu Kata wa Chadema kata ya Sokoni One na mmoja aliemtaja kwa jina la Justine mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa Sombetini ambaye alifariki katika hospitali ya Mkoa Mount Meru muda mfupi baada ya kufikishwa.

Kufuatia tukio hilo Msimamizi wa uchaguzi mdogo wa Madiwani katika kata nne za jimbo la Arusha,Sipora Liana ,ambaye ni Mkurugenzi wa jiji hilo, ametangaza kuahirisha uchaguzi huo uliokuwa ufanyike mapema jana hadi Juni 30 mwaka huu.

Alisema kuahirishwa kwa uchaguzi kutokana na hali tete iliyojitokeza na kusababisha uvunjifu wa amani, hivyo kwa mtizamo huo alisema isingewezekana kufanyika uchaguzi huo kutokana na hali ya usalama kuwa mdogo.

Aidha Mkuu wa mkoa alisema serikali imechukizwa na tukio hilo na imeapa kufanya uchunguzi na kuwabaini wahusika wa tukio hilo,akieleza kuwa tukio hilo linashabihiana na tukio la bomu lililotolea Mei 5 mwaka huu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Olasiti ambapo watu 3 walifariki wengine 67 kujeruhiwa.

Alisema matukio kama hayo hayavumiliki na anajisikia mnyonge kuona damu za watu wasio na hatia zikimwagika ovyo na kuwataka wakazi wa Arusha kuwa wavumilivu na watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola kuweza kutiwa mbaroni kwa wahusika wa ugaidi huo.

Mulongo alisema watu kadhaa wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio hilo na hali katika jiji la Arusha ni shwari na aliwasihi wananchi waendelee na shughuli zao wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi.

Akisimulia tukio hilo mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika hospitali ya Seliani, Abdalah Alila (39) alisema katika mkutano wa Chadema uliofanyika uwanja wa Soweto,Kaloleni jijini hapa,majira ya saa 11.50 jioni,aliona kitu cheusi kikidondo kakaribu yake na baadae alisikia mripuko mkubwa.

Alisema baada ya mripuko huo alijikuta akiwa chini na damu zikimchuruzika huku akishindwa kutembea na kuanza kutambaa akiomba msaada.

Tukio hilo limesababisha taharuki kubwa jijini hapa huku baadhi ya watu wakidai kuwa bomu hilo lililenga kumuua Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema.

Wakati huo huo, serekali imesema tukio hilo halikubaliki na sio la kibinadamu na kwamba linaashiria kuvuruga amani.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani Dk.Emanuel Nchimbi wakati alipotembelea eneo la tukio na kukutana na majeruhi katika hospitali za Seliani na Mount Meru.

Dk. Nchimbi alisema hadi sasa watu waliojeruliwa katika tukio hilo ni 70 ambapo kati yao wawili wamepoteza maisha na wengi wawili wapo mahututi.

Alisema serekali imepokea tukio hilo kwa masikitiko makubwa na kwamba halikubaliki na sio la kibinadamu.

Aidha alisema jeshi la polisi limetuma wapelelezi wa mabomu na upelelezi huo utasimamiwa na Mkuu wa operesheni wa jeshi hilo, Poul Chagonja huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola.

Wakati huo huo huko Monduli kata ya Makuyuni ambako kulifanyika uchaguzi wa Udiwani, Mbunge wa Arumeru, Joshua Nassari alipigwa na watu wanaosadikiwa kuwa mashabiki wa CCM na kuumia kwa matibabu zaidi.

Inadaiwa Mbunge huyo alipigwa na kulikimbia gari lake baada ya kutokea hali ya kutoelewana na vijana wa kata hiyo.

Wakati huo huo Mkuu wa jeshi la polisi, IGP Said Mwema ameteua jopo la wapelelezi inayoongozwa na Makamishna wawili wa Idara ya upelelezi kwenda Arusha.

Alisema polisi inaendesha operesheni kuhakikisha watu waliotekeleza, waliopanga na waliofadhi shambulizi hilo wanakamatwa.

Jiji la Arusha jana lilikuwa limezizima huku polisi wakionekana wakifanya doria kila kona ya jiji hilo.

Wakati huo huo Rais Kikwete ametuma salamu za rambi rambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kufuatia shambulizi hilo na kulitaka jeshi la polisi kuhakikisha liwatia mbaroni wahusika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.