Na Salum Vuai, Maelezo
WIZARA ya Afya, imewasihi wahitimu wa mafunzo ya afya katika Chuo cha Sayansi za Afya Mbweni, kutumikia nchi yao, badala ya kukimbilia nje kwa madai ya kufuata maslahi bora.
Akihutubia mahafali ya 20 ya chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo, Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, aliwataka wahitimu hao kuthamini walichonacho na kubaki nchini kuisaidia jamii yao ambayo inahitaji huduma zao.
Alisema serikali inathamini mchango unaotolewa na wafanyakazi wa sekta ya afya, na pia inajitahidi kuyafanyia kazi madai yao ya maslahi bora kila inapopata nafasi kwa mujibu wa bajeti yake.
Akizungumzia matatizo yaliyoelezwa na wahitimu hao ambayo walisema yanawakabili chuoni hapo, Duni alisema sio lengo lake wala la serikali kuyaviza madai yao, lakini anayachukulia hayo kama changamoto na kwamba yamempa upeo mkubwa wa kuijua zaidi taasisi hiyo.
“Mlipoanza kusoma mlikuwa hamna bei, lakini sasa madhali mmehitimu bila shaka thamani yenu imeongezeka, lakini eleweni kuwa kufikia ukubwa na kupata mishahara minono ni safari ndefu inayohitaji uvumilivu, mambo hayaji haraka kama mnavyofikiria,” alieleza Waziri Duni.
Alisema faraja ya madaktari ni kuona wagonjwa wanaowatibu wanapona, na si kufikiria kupata utajiri, ingawa alikiri nao wanahitaji maisha ya faraja, kulingana na jasho lao.
“Mwalimu ndiye anayewafundisha wataalamu wa kila fani ikiwemo udaktari, lakini sijapata kusikia mwalimu katajirika kwa ualimu wake. Kazi hii pamoja na udaktari ni za pekee na kama mtu anawaza kutajirika, basi hospitali hapamfai,” alisisitiza Duni.
Hata hivyo, aliwataka wahitimu hao kuwa tayari kufanya kazi popote katika visiwa vya Unguja na Pemba, kwa bidii na moyo, huku akiahidi kuhakikisha nafasi za ajira kwao zinapatikana haraka iwezekanavyo.
Alisisitiza haja kwa wataalamu wa afya kuzingatia maadili ya kazi zao, na kutaka roho zao wakiwa kazini na nje ya kazi, zifanane na weupe wa sare zao.
Katika hatua nyengine, Duni alisema wizara yake italipa kipaumbele suala la kuwaendeleza walimu kielimu, kwa kuwa hilo ni miongoni mwa mikakati ya Wizara ya Afya na chuo hicho hadi kufikia kutoa wataalamu katika ngazi ya shahada ya kwanza.
Aidha alisema serikali inaelewa fika kwamba mazingira bora ya kazi, huleta ufanisi zaidi kwa walimu ili wanafunzi waweze kusoma vizuri.
“Mwalimu anahitaji utulivu wa kimwili na kiakili. Hivyo basi suala la ‘scheme of service’ kwa chuo, wizara inalifanyia kazi. Nafurahi kuwa hivi sasa chuo kinayo mamlaka yake, yaani ‘autonomy’ ili kuyapunguza kama si kuyaondoa kabisa matatizo ya maslahi ya wafanyakazi wake kwa mujibu wa sheria namba 10 ya mwaka 1998 iliyokianzisha,”alifafanua.
Mapema, wakisoma risala, wahitimu hao walieleza changamoto mbalimbali ambazo Waziri Duni aliahidi kuzitafutia ufumbuzi hatua kwa hatua, ili kuweka mazingira mazuri ya kusoma na kufanya kazi kwa wanafunzi na walimu wa chuo hicho.
Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa vifaa vya kusomeshea, vikiwemo vya maabara na maktaba, kuongeza mabasi kwa ajili ya usafiri wa kwenda chuoni, kumalizia ujenzi wa ukuta unaokizunguka chuo hicho.
Aidha kuhusu tatizo la kuvamiwa kwa eneo la chuo hicho, Duni alisema bado liko mahakamani kutokana kesi iliyofunguliwa na baadhi ya watu kupinga hatua ya wizara kuamua kujenga ukuta ili kulihami, hivyo akasisitiza subira wakati kadhia hiyo ikiendelea kusikilizwa.
Mapema, Mkuu wa chuo hicho Dk. Haji Mwita Haji, akitoa mchanganuo wa taaluma chuoni hapo kwa ngazi ya cheti na stashahada, alisema jumla ya wanafunzi 408 wamefanikiwa katika fani mbalimbali.
Alizitaja fani hizo kuwa ni, ukunga,afya ya jamii, maabara, uuguzi, afya ya kinywa na meno, maafisa tabibu, afya ya mazingira, madawa na uuguzi ukunga.
No comments:
Post a Comment