Habari za Punde

Mwenyekiti Wazazi ahimiza amani

Na Mwantanga Ame
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi, Abdalla Majura Bulembo amewataka wanachama kudumisha amani na kuachana na uchochezi utakaosababisha kuvunjika Muungano.

Aliyasema hayo katia uwanja wa mpira cha Matemwe Mkoa wa Kazikazini ‘A’ Unguja.

Alisema hivi sasa ni lazima wanachama wawe makini kwa kutoa hoja zitakazofanya Muungano uliopo uendelee kubakia.

“Hivi vinavyotokea ni vijimambo tuu vinapita isomeni rasimu vizuri na muwe na hoja nzuri za kudumisha Muungano kuna watu wanataka shirikisho, wanataka benki ziangalieni hoja zao na muwe na hoja za msingi ili kudumisha Muungano wetu,” alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema Tanzania haiwezi kuona wananchi wake wanaingia katika matatizo na mifarakano jambo ambalo linaweza kuwaweka wanawake katika hali mbaya kwa vile ndio waathirika wa uvunjifu wa amani. “Sumu haijaribiwi anaetaka kuijaribu sumu huyo ana matatizo na ndio maana Mwalimu Nyerere katika uhai wake wote alikuwa anahubiri amani na wasiotaka hilo hao sio watu wema,” alisema .

Mapema Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Kaskazini, Haji Juma Haji, akimkaribisha mgeni rasmi, aliwataka wanachama wa CCM kutobabaika na watu wanaodai kutetea Wazanzibari.

Alisema msimamo wa Chama cha Mapinduzi, hadi sasa ni mfumo wa Serikali mbili kwa vile sera ya chama hicho haijabadilishwa na wanaodai mabadiliko ya serikali ya mkataba wanatokana na CUF, na sio Wazanzibari.

Mapema mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ali Ameir Mohammed, amewataka wanachama wa CCM kuendeleza mfumo wa muungano wa serikali mbili, kwani wanaodai muungano mkataba ni wasaliti wa Mapinduzi.

Alisema hashangai kuona kuna viongozi walioanza kuwashawishi watu kukubali mfumo wa muungano wa mkataba, kwani wenye mawazo hayo ndio waliowahi kujitokeza kutaka kusaliti Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema Wazanzibari ni lazima walitambue hilo na kuachana na ushawishi huo kwani walishawahi kutumia hila za aina hiyo kwa dhamira ya kutaka kuvunja muungano.

Alisema muungano unaoendelea kuungwa mkono na ni vyema wanachama wa CCM kuona maoni yao katika rasimu ya katiba mpya wanapigania kubaki kwa utaratibu huo.

Alisema kamati inayodaiwa kuteuliwa kufanya maridhiano haina msingi wowote wa kutaka kudumisha amani na inaonekana kufanya kazi zaidi ya kutaka kuvuruga nchi.

Aliwataka wanachama hao kuendelea kusimamia amani ya nchi ili kuifanya serikali kutekeleza majukumu yake vyema.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wanachama mbali mbali wa CCM akiwemo mke wa Makamu wa Pili wa Rais, mama Asha Seif Iddi, na Wenyeviti wa mikoa ya CCM ya Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.