
Na Raya Hamad
Imeelezwa
kuwa moja kati ya neema alizopewa mwanaadamu ni umri mrefu hivyo ni wajibu wa
kila mmoja wetu kuutumia vyema uhai wake kwa kutenda mema na kushukuru kila
siku kwani hapaswi mwanaadamu kuwa aasi bali anachotakiwa ni kumuabudu Mola
wake aliyemuumba .
Kadhi
mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji Khamis ameyasema hayo katika dua ya
kumshukuru Mwenyezi Mungu kutimiza miaka
93 ya kuzaliwa kwa Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Alhajj Aboud
Jumbe Mwinyi iliyofanyika Kiembe Samaki
.
Sheikh
Khamis Haji ametowa ukumbusho kwa kusema kuwa “ Ifanye dunia kama kwamba
utaishi milele kwa maana ya kutenda mazuri na kumuabudu Allah kama tulivyoamrishwa katika dini pia ifanye akhera
yako kama utakufa sasa kwa maana ya kujiandaa kwa kutenda amali njema na kuomba
msamaha kila siku .
Katika
khutba yake iliyosomwa na Ustadh Moh’d Yoyota kwa niaba yake Rais Mstaafu Awamu
ya Pili Alhajj Aboud Jumbe amesema kuwa
anamshukuru Mola wake kwa umri
aliyomjaalia kwani ameshuhudia neema nyingi ambazo hazina kiima
kisicho kifani,kina wala mizani katika
maisha yake na kupitia nyanja tofauti za maisha hadi M/Mungu
atakapomjaalia mwisho wa maisha yake.
Alhajj
Aboud Jumbe ameongeza kusema kuwa anamshukuru Mola wake kwa kumpa rehema zake
huruma na hisani pale alipokabidhiwa dhamana ya kuongoza baadae kumnusuru na kumfariji na hatimae kumuongoza
pale alipoteleza mnamo asiyoyaridhia kwani majibu sahihi ya mithani yetu wanaadamu
yanasubiri siku ya malipo ambayo yatupasa tutambue kuwa kila mmoja wetu
atakutana nayo.
“Namuomba
Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu azidi kuitakasa amali yangu na kunipa khusni l
khatima mimi pamoja na waislamu wenzangu “
Akitowa
shukurani kwa waalikwa waliohudhuria katika dua hiyo kwa niaba ya familia ndugu Mustafa
Aboud Jumbe ambae ni mtoto wake amesema kuwa lengo la kusoma dua hii ni
kukumbushana namna gani tunatumia neema na kila mmoja vipi atautumia uhai wake
na kusisitiza kuwa dua hio ni mwenyewe baba yao aliyetowa utaratibu juu ya
namna gani isomwe dua hio “Tumekuwa tukipata masuala mengi kuhusu hali ya mzee wetu
jibu ni kwamba hajambo ila uzee tu ndio unaomsumbua, nuru ya macho
imepotea ,kusikia kumekuwa shida kidogo lakini anasikia na anazungumza na hii
shughuli yake ya leo amepanga mwenyewe”alisisitiza
Mustafa Jumbe.
Nae
Sheikh Moh’d Iddi ametowa wito kwa jamii
kufanya matendo mema kwani kuwepo kwetu ipo historia ambayo M/ Mungu
amewashushia waja wake na aliyebahatika kuishi kwa kumuabudu huyo atakuwa
amefaulu.
Miongoni
mwa waliohudhuria katika dua hio ni
pamoja na Kadhi Mkuu Mstaafu Sheikh Habib Ali Kombo baadhi ya Masheikh, Familia
yake, baadhi ya wanafunzi aliwahi kuwasomesha na kuwafundisha kazi .
No comments:
Post a Comment