HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA MAENDELEO YA WANAWAKE NA
USTAWI WA JAMII KUHUSIANA NA BAJETI YA WIZARA YA AFYA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote hatuna budi
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku uhai na Afya njema na kutuwezesha
kukutana tena leo hii kwa madhumuni ya kuwatumikia wananchi wetu na manufaa ya
taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
Pili napenda nikushukuru wewe
binafsi kwa kuniruhusu kusimama mbele ya Baraza lako tukufu kwa niaba ya Kamati
ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii kuwasilisha maoni ya Kamati
kuhusiana na makadirio ya mapato na matumizi ya kazi za kawaida na maendeleo
kwa mwaka wa Fedha 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua nafasi hii
kumshukuru Waziri wa Afya, Naibu Waziri, pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa
mashirikiano yao waliyotupa wakati wa kupitia na kuichambua bajeti ya Wizara,
kwa kweli mashirikiano yao yamefanikisha kumaliza kazi hii kwa wakati na kwa
ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Sitokuwa nimetenda haki hata kidogo
iwapo nitakosa kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya
Wanawake na Ustawi wa Jamii kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi kuniwezesha leo
hii kusimama mbele ya Baraza lako tukufu kuwasilisha maoni ya Kamati juu ya
makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa Fedha 2013/2014. Naomba niwatambue
kwa kuwataja majina wajumbe wa Kamati kama
hivi ifuatavyo:-
1.
Mhe.
Mgeni Hassan Juma Mwenyekiti.
2.
Mhe.
Hassan Hamad Omar M/Menyekiti.
3.
Mhe.
Abdi Mosi Kombo Mjumbe.
4.
Mhe.
Ali Salum Haji Mjumbe.
5.
Mhe.
Farida Amour Moh'd
Mjumbe.
6.
Mhe.
Mwanaid Kassim Mussa Mjumbe.
7.
Mhe.
Mohamed Mbwana Hamad Mjumbe.
8.
Ndg.
Maryam Rashid Ali Katibu.
9.
Ndg.
Asha Said Mohamed. Katibu.
Mheshimiwa Spika, Baada ya utangulizi huo, naomba
kutoa maoni ya Kamati kuhusiana na Bajeti ya Wizara ya Afya.
Jengo la Ofisi Kuu – Pemba.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imesikitishwa na hali ya Wizara ya Afya Pemba Kukosa ofisi
yake. Ofisi kuu Pemba imekuwa haina jengo kwa
muda mrefu na inatumia chumba kimoja kidogo kilichopo katika hospitali ya Wete;
hali ambayo hairidhishi kwani chumba hicho kinakuwa hakikidhi haja kwa matumizi
ya wizara nzima. Afisa mdhamini anashindwa kuwa karibu na wasaidizi wake mbali
mbali kutokana na ufinyu wa Ofisi.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaiomba Serikali kutatua tatizo la Of
isi ya wizara Pemba. Kiukweli Kamati haikuridhika na hali ya ufinyu wa
Ofisi kwasababu utekelezaji wa majukumu ya Wizara unakuwa ni ngumu.
Upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba katika Hospitali na Vituo vya Afya
Pemba.
Mheshimiwa Spika, Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni muhimu katika hospitali na vituo
vya afya; lakini Kamati ilipotembelea vituo vya afya na hospitali mbali mbali
ilibaini upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba. Sambamba na hilo,
Kamati ilifanya mahojiano na timu nne za afya Pemba
zilizopo katika Wilaya ya Micheweni, Wilaya ya Wete, Wilaya ya Chakechake na
Wilaya ya Mkoani; nazo zilikiri kuwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni
tatizo katika wilaya zao.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa huduma za afya na dawa, Kamati inaishauri Wizara
kutafuta kampuni nyingine ya kuagiza na kuingiza dawa nchini badala ya
kutegemea Ghala kuu ya Dawa ya Dar es Salaam pekee MSD (Medical Store of Dar es Saalam) ambao
nao huchangia uhaba wa upatikanaji wa dawa katika hospitali na vituo vyetu vya
afya katika muda unaotakiwa.
Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Kamati haikuridhishwa na utekelezaji
wa miradi unaondeshwa na wizara. Katika bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha
2012/2013 wizara ilijipangia kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo. Kamati
imebaini utekelezaji usio wa ufanisi katika programu shirikishi ya afya ya mama
na mtoto, mradi wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na mradi wa kuvipandisha
hadhi vituo vya huduma za afya. Malengo ya miradi hiyo hayakuweza kufikiwa
kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Katika utekelezaji wa programu shirikishi ya afya ya mama na mtoto
ambayo ilikusudia kujenga vyumba vya baridi na kufanya ukarabati wa ofisi ya
chanjo Pemba, Kamati ilisikitishwa sana
kuwa utekelezaji wake haukuweza kufanyika, na hakukuwa na sababu za msingi kwani
fedha za wahisani ziliingizwa na kushindwa kufanyiwa kazi katika muda
uliokusudiwa. Kitendo hichi ni kuwavunja moyo wahisani wetu na Kamati inamtaka
Waziri atoe maelezo juu ya jambo hili.
Mheshimiwa Spika, Pia Kamati inaiagiza
wizara katika utekelezaji wa Bajeti
ya mwaka 2013/2014 kuhakikisha kuwa wanafanya ujenzi wa haraka wa vyumba vya
baridi pamoja na ukarabati wa Ofisi ya chanjo, kwani chanjo zote kwa upande wa
Pemba zinahifadhiwa katika ofisi hiyo, kuendelea kuchelewa kufanya ujenzi
kutapelekea kutokuwa na uhakika wa usalama wa chanjo zetu pamoja na wafanyakazi
wanaohudumia ofisi hiyo.
Mheshimiwa Spika,katika Mradi wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, Wizara ilikusudia
kufanya matengenezo katika vituo vya afya vya Mzambarauni na Wesha kwa Upande
wa Pemba na kwa Unguja Kituo cha Afya Mwera.
Vituo vyote hivyo vilikosa kukarabatiwa katika Kipindi husika, ukarabati
uliofanyika ni wa kituo cha Afya cha Bogoa pekee ambacho utekelezaji wake
ulikuwa wa tangu bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012.
Mheshimiwa Spika, Aidha katika mradi wa kuvipandisha hadhi vituo vya huduma za afya,
lengo lake lilikuwa ni kufanya utanuzi wa majengo
ya Hospitali ya Kivunge na Micheweni pamoja na ununuzi wa vifaa mbali mbali kwa
ajili ya utoaji mzuri wa huduma za afya katika hospitali hizo. utekelezaji wake
haukuwa wa kuridhisha.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaitaka Serikali kuingizia fedha Wizara kwa Wakati ili iweze
kutekeleza mipango yake iliyojipangia
ikiwemo utekelezaji wa miradi
kwa lengo la kuimarisha huduma za afya nchini na kuinua sekta hii muhimu.
Idara ya Utumishi na uendeshaji.
Mheshimiwa Spika katika mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ilikamilisha mpango mkuu wa
mafunzo kwa wafanyakazi ambao utekelezaji wake utaanza kutumika rasmi katika
mwaka huu wa fedha. Kamati inaipongeza Wizara kwa kuweza kukamilisha mpango huo
muhimu ambao utasaidia katika kupunguza upungufu mkubwa wa wafanyakazi wa afya
katika kada mbali mbali kwa hospitali na vituo vya afya.
Mheshimiwa Spika Katika nchi yetu tumekuwa na upungufu mkubwa wa madaktari wa magonjwa
ya akili, madaktari wa X-ray, madaktari wa magojwa ya damu na madaktari wa
kensa.
Kamati inaishauri Wizara katika
mpango mkuu wa mafunzo kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kuwahimiza wafanyakazi
watakaoenda masomoni kuchukua fani zilizokuwa pungufu katika nchi yetu na pia
kuwepo na motisha maalumu kwa watakaokubali kuchukua fani hizo.
Mheshimiwa Spika, pia Kamati inaisititiza Wizara kusimamia vyema mfumo wa takwimu za
rasilimali watu, mfumo ambao husaidia katika kupangia wafanyakazi sehemu za
kazi kwa mujibu wa mahitaji.Wizara imekuwa inakabiliana na changamoto ya
wafanyakazi wengi wa afya kutopendelea
kufanya kazi vijijini na badala yake kupendelea zaidi kubakia mijini pekee.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaiomba Wizara ijitahidi kusimamia maslahi ya wafanyakazi na
ihakikishe inasimamia ipasavyo mapendekezo ya rasimu ya maposho kwa wafanyakazi
wanaofanya kazi katika mazingira ya hatarishi na pia kuwazingatia wale
wanaofanyakazi katika mazingira ya vijijini yaliyokosa huduma muhimu. Kufanya
hivyo kunaweza kuwavutia wafanyakazi wetu kubakia katika ajira na kupunguza
idadi kubwa ya wafanyakazi wanaokimbia kufanya kazi vijijini na katika nchi
yetu kwa jumla.
Idara ya Sera, Mipango na Utafiti.
Mheshimiwa Spika, Kamati inapongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na idara katika
mchakato mzima wa kuanzisha bima ya afya kwa wananchi. Kiukweli bima hiyo ni
muhimu na itawasaidia wananchi kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya kila
watakapokuwa wanasumbuliwa na maradhi mbali mbali.
Mheshimiwa Spika, Kumekuwa na wananchi ambao hushindwa kuhudhuria katika hospitali na vituo
vya afya kutokana na kushindwa kumudu gharama za afya. Kamati ina matumaini
makubwa kwamba kuanzishwa kwa bima ya afya kutawawezesha wananchi walio
wanyonge kufaidika na huduma za afya kwa kadri watakavyokuwa wanazihitajia.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaisisitiza Wizara
kuendelea na hatua mbali mbali zinazohusiana na kukamilika kwa bima hiyo na pia
kuandaa utaratibu mzuri ambao utapelekea kupatikana kwa huduma kwa wepesi na
kunufaisha wananchi wote.
Idara ya Kinga na Elimu ya Afya.
Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa majukumu ya Idara ni kukinga na kukabiliana na maradhi ya
kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza. Katika miaka ya hivi karibuni, katika
visiwa vya Zanzibar kumekuwa na ongezeko kubwa
ya magojwa yasio ya kuambukiza ikiwemo shindikizo la damu, kisukari, saratani
na magojwa mengine sugu ya mapafu kama vile
pumu.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Wizara kwa kuweza kufanya utafiti katika hospitali
nne za vijiji na hospitali tatu za Wilaya na kuweza kubaini hali halisi ya
magojwa na kutambua mahitaji ya taaluma, vitendea kazi na rasilimali watu.
Mheshimiwa Spika, Kitengo cha kupambana na magojwa yasio ya kuambukiza kinaendelea
kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na magojwa hayo na Kamati
inaisisitiza wizara, pamoja na kuwepo kwa kitengo, kuendelea kuusimamia
muongozo wa matibabu ya magojwa yasioambukiza ili uweze kukamilka na kuanza
kutumika.
Mheshimiwa Spika, Aidha kwa upande wa maradhi ya malaria, Kamati inapenda kuipongeza Wizara kwa jitihada wanayoendelea
kuchukua ya kudhibiti maradhi hayo. Kamati iliweza kujionea wenyewe kisiwani Pemba shehia ya Tumbe kuwa ugojwa wa malaria katika kijiji
hicho umeweza kutokomezwa. Kamati inaiomba Wizara kuendelea na juhudi ya
kudhibiti maradhi ya malaria ili yasije yakaibuka tena kwa kuendela kutoa elimu
ya kinga ya maradhi hayo.
Mheshimiwa Spika, Kamati ina matumaini makubwa kuwa Idara itaendelea kufanya vizuri
katika majukumu yake mbali mbali kutokana na ongezeko la bajeti kutoka milioni
mia mbili thalathini na moja (231,000,000) katika mwaka wa fedha 2012/2013
mpaka kufikia milioni mia tatu hamsini (350,000,000) katika mwaka huu wa fedha.
Idara ya Tiba.
Mheshimiwa Spika, Idara hii inajumuisha hospitali za
Wilaya na Vjiji na pia inasimamia mradi wa kupandisha Hospitali za vijiji na
wilaya. Kiujumla hospitali zetu zinakabiliana na changamoto za msingi ikiwemo
hali mbaya ya upatikanaji wa dawa na vifaa, uchakavu wa majengo, uchache wa
wafanyakazi, kuwepo kwa madeni makubwa ya maji na umeme, kukosekana kwa uzio
katika vituo vya afya, walinzi nakadhalika.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaitaka Serikali kuisadia wizara katika kukabiliana na
changamoto hizi.Kamati imeweza kushuhudia uchakavu na ufinyu wa majengo katika
hospitali zetu za vijiji na wilaya. Kwa upande wa hospitali ya vitongoji Pemba, maabara, wodi na nyumba za madaktari zimekuwa ni
chakavu na hali ya upatikanaji wa dawa
na vifaa sio mzuri.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaona kama kweli ile adhma ya
Serikali ya kuzipandisha hospitali za vijiji kuwa za wilaya, na zile za wilaya
kuwa za mkoa inafikiwa lazima Serikali ihakikishe inaongeza fedha, majengo,
vifaa na vitendea kazi katika hospitali hizo.
Mradi wa Kuimarisha Huduma za Afya Wilayani.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huu unategemea ufanisi mkubwa wa Timu za afya za
wilaya pamoja na mfumo ulioanzishwa na Wizara wa kuendesha kazi za timu za
wilaya ambapo mfuko maalum wa pamoja wa fedha( District Health Services Basket
Fund) hutumika katika kuwapatia fedha timu hizo.
Mheshimiwa Spika, Kamati imegundua kuwa utaratibu unaotumika wa kuwapatia fedha timu za Afya
za wilaya bado haujafahamika kwa timu zewenyewe na hivyo kupelekea timu hizo
kukosa fedha kwa wakati. Kamati inaiomba Wizara kuendelea kutoa elimu juu ya
mfumo ulioanzishwa ili maafisa wa timu za afya za wilaya wapate fedha kwa
wakati na pia wapewe madaraka ya kuzitumia fedha kwa kufanikisha kazi zao.
Mheshimiwa Spika, timu za afya za wilaya zimeweza kufikia vituo mbali mbali vya afya na
kuona utekelezaji wa huduma zinazotolewa katika vituo. Mbali na jitihada za
kufikia vituo hivyo, timu hizo ziliweza kugundua changamoto zilizopo kama
ufinyu wa vituo, upungufu wa wafanyakazi, kukosekana kwa uzio katika vituo,
madeni makubwa ya umeme na maji, matokeo ya uvamizi na wizi na ukosefu wa vifaa
tiba.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaiomba Serikali kuisaidia wizara katika kuzitafutia ufumbumbuzi changamoto
hizo ili hatimae huduma za afya za wilayani ziweze kuimarika.
HITIMISHO:
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya kwa bajeti ya mwaka 2012/2013 imepata mafanikio katika
baadhi ya maeneo huku ikiwa bado baadhi ya maeneo yanahitaji kufanyiwa kazi.
Kamati yetu kiujumla haijaridhika kabisa na uingizwaji wa fedha katika Wizara
ya Afya kwa matumizi ya kazi za kawaida na kazi za maendeleo. Uingizwaji wa
fedha usioridhisha unaendelea kuikwamisha wizara katika kutekeleza majukumu
yake. Hivyo Kamati inaiomba Serikali kuipa kipaumbele wizara kwa kuingizia
fedha ipasavyo ili iweze kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, nawaomba wajumbe wenzangu wa Baraza lako
Tukufu, kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2013/2014
Jumla ya Tshs 21,318,000,000 (Bilioni
ishirini na moja na milioni mia tatu kumi na nane) kwa kazi za kawaida, Ruzuku,
Mishahara na maposho na Tshs 6,333,000,000( bilioni sita, milioni mia tatu na
thalathini na tatu)kwa kazi za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana
kwa kunisikiliza na kwa niaba ya Kamati naunga mkono hoja na naomba
kuwasilisha.
Ahsante.
..............................
Mhe.
Hassan Hamad Omar
Kny:Mwenyekiti,
Kamati ya
Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii.
Baraza la
Wawakilishi,
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment