Habari za Punde

Hutuba ya Mhe. Rais wa Zanzibar kuukaribisha Mwezi wa Ramadhani.


RISALA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. ALHAJ DK. ALI MOHAMED SHEIN,

JULAI, 2013, RAMADHAN 1434 A.H.

 

BISMILLAHI RAHMAN RAHIM.
Namshukuru Mwenyezi Mungu Karim, Mwenye wingi wa Rehema, aliye muweza wa kila kitu.  Yeye ndiye mwenye kustahiki shukurani za waja wake na viumbe vyote.

Ndugu Wananchi,

RAMADHANI KARIM,

Assalam Alaykum wa Rahmatullahi Wabarakatuhu,
Tumefikiwa na mwezi Mtukufu wa Ramadhani.  Hatuna budi waumini sote kwa pamoja tumshukuru Mola wetu kwa kutupa uhai na tukaweza kuukaribisha mwezi huu.  Namuomba  Muumba wetu atuzidishie umri na afya ili tuweze kuukaribisha mwezi huu katika ibada kwa salama na amani.  Na atufikishe kwa kheri na salama miezi mengine ijayo mwaka baada ya mwaka.

Ndugu Wananchi,
Kufikiwa na mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni neema kubwa kwetu.  Huu ndio mwezi ambamo waumini tumepewa ibada ya kufunga, Saumu, tukateremshiwa kitabu kitukufu cha uongofu, Qurani katika usiku wenye heshima kubwa, Lailatul Qadri. 

Haya yameelezwa na mwenyewe Subhana Wataala katika Qurani Surat Al-Baqara aya ya 183 mpaka 187 yenye maelezo ya kina juu ya ibada hii ya kufunga. Maimamu na Masheikh wanazieleza aya hizi katika khutba za Ijumaa na kwengineko.

Ndugu Wananchi,
Inafaa tukumbushane na kupeana mafunzo kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amefaradhisha ibada ya Saumu iwe ni njia kubwa kwetu ambayo tukifuata tutapata kuongoka na kuzipata rehema za Mola wetu (SW).

Ibada hiyo inatupa mazoezi ya kufanya vitendo kwa nia na moyo safi, yaani IKHLAS na ustadi.  Vile vile, inastawisha sifa ya mtu kuwa na nidhamu ya nafsi inayopelekea atekeleze vilivyo wajibu wake na kumzuia kufanya maasi na yote aliyokataza Mola wetu.   Tunafunga bila ya ria na Mola wetu ndiye anaeziona Saumu zetu.
Bwana Mtume amepokea kutoka kwa Mola wake, hadithi Qudsi, inayosema:-

  “Ikhlas ni siri nimeitia moyoni mwa mja wangu, hapana malaika atakayejua ila aiandike, au shetani ili aiharibu”

Ni kwa sababu hiyo ndio Mtume Muhammad (SAW) akatuambia kwamba Mola anasema:-

          “Saumu ni kwa ajili yangu na mimi ndiye ninaelipa”

Hiyo ni neema na kheri kubwa.

Ndugu Wananchi,
Hii Ikhlas ndiyo inayotufunza kufanya mema na kuyabeza maovu, tukitambua kuwa Mwenyezi Mungu anatuona kwa kila tunalofanya au kudhamiria kulifanya, ikiwa la kheri au la shari.

Kwa kauli ya Mtume Muhammad (SAW)

  “ Wema ni kumuabudu Mwenyezi Mungu kama kwamba unamuona; kwa sababu kama wewe humuoni yeye anakuona”

Vile vile, katika sifa mojawapo za Mwenyezi Mungu ni kuwa:-

          “Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila jambo ni shahidi”

Katika Quran, Surat Al-Nakhl, Aya ya 19, Mwenyezi Mungu amesema:

  “Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyaficha na mnayoyatanguliza”

Pia katika Surat Isra, Aya ya 25 Mola anatuambia:

  “Mola wenu anajua kabisa yaliyo nyoyoni mwenu.  Ikiwa mtakuwa wema, basi hakika Yeye ni Mwenye kuwaghufiria wanaotubu kwake”.
Ndugu Wananchi,
Katika kutafakari hayo, tujue kwamba Ramadhani imetufikia ili tutafute na kupata sifa za usafi wa nia na utu wema.  Tumo katika kipindi chenye harakati za kidunia na wakati mwengine tunasahau mwisho wetu.  Ni kweli kwamba Bwana Mtume Muhammad (SAW) ametuambia:-

“Fanya mambo ya kheri kwa dunia yako kama kwamba utaishi milele”

Lakini pia ameongeza kwa kusema :-

          “Na fanya kheri kwa Akhera yako kama kwamba utakufa kesho”
Hasa katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani inatupasa tuzifuate sifa zote  tulizofunzwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, tuondoe sababu zote za utengano na mfarakano na tuimarishe njia zote za umoja, ushirikiano, ihsani na kupendana.

Tukifanya hivyo tutakuwa tumewajibika kwa Mola wetu pamoja na kupata malipo yake ya kheri ya Ramadhani na amani itaenea, usalama utazagaa, maisha yatastawi na wananchi tutazidi kuneemeka.

Ndugu Wananchi,
Mashekh wetu wanatufunza kuwa Mwenyezi Mungu ameichagua na kuitukuza Ramadhani iwe ni wakati wa kujizoesha kufanya mema ili baadae iwe ndio tabia yetu ya kawaida.  Katika mwezi huu tunahimizwa kuongeza ibada ya Sala kwa kusali Tarawekh na Sala nyengine za Sunna hasa nyakati za usiku.   Tumehimizwa kusameheana, kutoa sadaka zaidi na kuwa wapole na kujikinga na maovu yote ambayo yanavunja Saumu, Bwana Mtume (SAW) ametuelekeza:-

          “Mche Mungu na uongoke kwa vitendo vyema”.
Tuhimizane kufanya mema na tumche zaidi Mola wetu.
Ndugu Wananchi,
Napenda kugusia machache ambayo yamehusiana na Rehema, hasa katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani. Nakumbusha kwamba wakati tunatafuta riziki katika mwezi huu tuzingatie haki na kurehemiana sana katika biashara, hasa muuzaji na mnunuzi.

Tunatambua kwamba faida kwa mfanyabiashara ni lazima, ili aweze kujimudu na kuendelea.  Lakini wakati huo huo Mwenyezi Mungu anatwambia katika Qurani Tukufu Suratu An Nisaa Aya ya 29.

  “Enyi mlioamini msiliane mali zenu kwa batili (dhuluma) isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu”
Aya hii inatudhihirishia tufanye biashara ya haki, bei ziwe za haki na bidhaa ni nzuri sio za kuhadaiana.  Kwa upande wa Serikali hatutavumilia kuona watu wanahatarisha maisha na afya ya wengine kwa kuwauzia bidhaa zilizopitwa na wakati, mbovu na zisizokuwa na vipimo bora.  Kwa upande wa mazao ya kilimo, kama ndizi zinazouzwa zikiwa changa.  Naagiza vyombo husika kuchukua hatua madhubuti kuhusu hayo niliyoyataja juu ya biashara.  Inafaa tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia baraka ya mazao ya aina nyingi ya kilimo wakati huu na vile vile, nawashukuru wafanyabiashara wetu kwa kujaza madukani mwao bidhaa mbali mbali zinazohitajika zaidi katika mwezi huo, zikiwemo vyakula na nguo.

Ndugu Wananchi,
Natoa wito kwetu sote tuwe wenye kurehemeana kwa njia mbali mbali, hasa katika kutoa Sadaka.  Bwana Mtume Muhammad (SAW) amesema:-

          “Mwenyezi Mungu humsaidia mja anayemsaidia nduguye”

          na pia akaongeza kwa kusema:-

  “Mrehemu (Mfanyie ihsani) aliopo katika ardhi (duniani) na atakurehemu aliopo mbinguni”

Nawashukuru wakulima wetu Unguja na Pemba, kwa jitihada za kuzalisha mazao zaidi ya chakula. 

Basi tuwakumbuke kwa rehema wenzetu wasiojiweza, mayatima, masikini, wanafunzi waliopo dakhalia mbali mbali, wagonjwa waliopo hospitalini na watu wengine wanaohitaji kusaidiwa angalau kwa futari.

Ndugu Wananchi,
Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani umekuja wakati wa msimu wa utalii nchini kwetu.  Tutakuwa na wageni wengi na wengine wasiokuwa Waislamu.  Wao ni wasafiri na dini yetu inatufundisha kwamba Waislamu wawe na moyo mzuri kwa wasafiri.  Ni vyema kuwa na subira kuwaongoza juu ya taratibu, mila na kanuni zetu katika mwezi huu bila ya bughudha au uvunjaji wa sheria.

Wafanyabiashara wa vyakula, hotelini na mikahawani wanapaswa kuheshimu khulka, mila na utamaduni wetu.  Tusifanye mambo ya karaha na kuwakasirisha wanaofunga. Wasiofunga wawaheshimu wanaofunga.  Tufanye Ramadhani yetu iwe ni kivutio cha wageni, kwa utamaduni na ustarabu wetu.

Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia natoa wito kwa wananchi wote kuwa waangalifu na kutumia vyakula na maji bila ya israfu.  Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) itafanya kila juhudi ili kuhakikisha kuwa maji yanapatikana katika maeneo mbali mbali nchini mwetu. Tuitumie vyema neema anayotupa Mola wetu huku tukijua kuwa hapendi uharibifu.

Namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie Ramadhani ya mafanikio kwetu sote, kuanzia kwa wafanyabiashara, Wakulima, Wavuvi, Washoni, Waendeshaji darsa za dini, Vijana, Wazee na wananchi wote kwa ujumla.  Ewe Mola wetu tupe uongofu wako, ijaalie nchi yetu idumu na salama, amani, umoja, mshikamano na upendo kati yetu.


Ramadhani Karim,

Assalam Alaykum wa Rahmatullahi Wabarakatuhu,

 

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

                                                  

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.