Habari za Punde

Ajeruhiwa kwa Kuangukiwa na Ukuta

MTU mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Robert mkaazi wa Migombani amejeruhiwa vibaya baada ya kuangukiwa na ukuta alipokuwa katika shughuli za ujenzi wa ukuta wa kuzuia maji ya mvua katika eneo la Ngazi Mia, Migombani mjini Zanzibar.

Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa tano asubuhi wakati mtu huyo akiwa na mafundi wenzake walipokuwa wakijenga ukuta huo unaomilikiwa na Salim Mohammed Ahmed, ambao ulianguka ghafla na kumlalia.

Kwa mujibu wa mafundi waliokuwa katika shughuli za ujenzi wa ukuta huo walisema, ghafla ukuta huo ulipata ufa mkubwa na ndipo walipolazimika kuhimizana kukimbia, lakini Robert hakuwahi kuondoka na kumuangukia sehemu za kiunoni.

Juhudi za kumnasua kutoka kwenye ukuta huo zilifanikiwa baada ya muda wa takriban saa moja, kutokana na msaada mkubwa wa mafundi wenzake, wananchi waliokuwa wakipita katika eneo hilo, wafanyakazi wa ofisi zilizo jirani ya eneo la ujenzi, pamoja na askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi.

Mara baada ya kutolewa chini ya ukuta huo, Robert anayekisiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 40 alikimbizwa hospitali Kuu ya Mnazimmoja kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi muda mfupi baada ya kutokea tukio hilo huko kwenye eneo la tukio, mmiliki wa ukuta huo, Salim Mohammed Ahmed alielezea kusikitishwa na ajali hiyo na alikuwa katika harakati za kuhakikisha fundi huyo anapatiwa matibabu muhimu yanayohitajika.

Alisema aliamua kujenga ukuta huo kuzuia maji ya mvua ambayo yalikuwa yakishuka kwa kasi katika eneo hilo la ufukweni jirani na Ngazi Mia, ili kuzuia mmong’onyoko wa ardhi na kusababisha madhara kwa nyumba pamoja na ufukwe wa bahari.
Juhudi za kumpata msemaji wa Jeshi la Polisi kuelezea kwa undani mkasa huo hazikuweza kufanikiwa jana.

1 comment:

  1. Brither Othman bado wamo na unangara sikuamini macvho yangu Mungu akupe umri mfrefu wenye afya na madili mema ayapendayo

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.