Na Said Ameir, Ikulu
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ni wakati
muafaka kwa mahakama, vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria na jamii
barani Afrika kushirikiana kwa pamoja katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo la kuongezeka
kwa vitendo vya kihalifu barani humo.
Akizungumza katika
ufunguzi wa Mkutano wa kumi na moja wa Chama cha Majaji na Mahakimu cha Afrika
Mashariki(EAMJA) unaofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort leo Dk.
Shein amesema kumekuwepo na mjadala wa muda mrefu juu ya uhusiano wa ongezeko
la vitendo hivyo na ufanisi wa utendaji kazi katika vyombo vinavyosimamia
utekelezaji wa sheria.
“Kumekuwepo na
mijadala mingi kuhusu utendaji wa vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa Sheria
katika nchi nyingi barani Afrika na mingi ya mijadala hiyo inaonyesha kidole
udhaifu katika utekelezaji wa sheria ambao unaelezwa kuwa unachangia ongezeko
hilo la vitendo vya kihalifu” Dk. Shein.
Aliongeza kuwa tatizo
hilo linatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazokwamisha maendeleo barani Afrika.
Katika mnasaba huo,
Dk. Shein amewataka wanachama wa EAMJA kuendelea kufanyakazi kwa karibu na
vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria pamoja na jamii ili kuhakikisha
sheria zinatekelezwa ili haki iweze kutendeka.
Alivitaja baadhi ya
vitendo vya kihalifu ambavyo vitachukua nafasi katika mijadala ya mkutano huo
kuwa ni pamoja na rushwa na unyanyasaji watoto.
Dk. Shein
aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imejidhatiti kupambana na tatizo la rushwa nchini na imeunda mamlaka maalum ya
kushughulikia rushwa na uhalifu wa kiuchumi.
“Serikali
imeanzsiha Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhalifu wa Kiuchumi na tumekuwa
tukifanya jitihada kubwa kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya rushwa,
uhalifu wa kiuchumi na umuhimu wa kuzingatia maadili” Dk. Shein alifafanua.
Kwa hiyo ameeleza
matumaini yake kuwa mkutano huo wa siku tano utakuwa wa manufaa sana kwa
Zanzibar kwa kuwa utaimarisha ujuzi na ufahamu wa wataalamu wa sheria wa
Zanzibar ambao ni miongoni mwa washiriki.
Akizungumzia kuhusu
kaulimbiu ya mkutano huo ambayo ni ‘Haki ya kuishi: mtazamo na changamoto’ Dk.
Shein alikiri kuwa baadhi ya masuala yatayozungumziwa chini ya kaulimbiu hiyo
yanayoweza kugusa imani za kidini na hata itikadi za watu hivyo aliwataka
washiriki wasiongozwe tu na taaluma bali kuzingatia mila, silka na utamaduni wa
Afrika.
“Katika mijadala
yenu ningewaomba muzingatie utamaduni na silka za watu wa Afrika. Si kila kitu
kizuri kwa jamii nyingine kwa mfano Ulaya na Marekani lazima kiwe kizuri kwetu
sisi Afrika” aliwasihi na kuongeza kuwa mijadala na maazimio ya mkutano huo ni
vyema yazingatie tamaduni za nchi za Afrika
Mashariki.
Katika mkutano huo
miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa na kutarajiwa kuzua mjadala mkubwa ni
pamoja na hukumu ya kifo na suala la utoaji mimba. Masuala hayo yamekuwa
yakichukua nafasi kubwa katika mijadala mbalimbali ya kisheria kutokana na
kuwepo mitazamo tofauti na hoja mbalimbali zinazokataa au kuunga mkono zote
zikihusisha haki za binadamu.
Dk. Shein
ameishukuru EAMJA kwa kuiteua Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kueleza uamuzi
huo unathibitisha imani ya wanachama wake kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa.
“Uteuzi wenu za
Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano huu unathibitisha imani ya wanachama wa EAMJA
kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa”
Dk. Shein alibainisha.
Ameongeza kuwa
mkutano huo unafanyika katika kipindi muhimu cha historia ya Zanzibar kwa kuwa
ndio inaelekea kuadhimisha mika 50 ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari,
1964”alisema Dk. Shein na kubainisha kuwa “ ni wakati mzuri kushirikiana na
majirani zake hivyo mkutano huu ni mwanzo mzuri”
Wakati
huo huo Chama cha Mahakimu na Majaji cha Afrika
Mashariki kimeishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake
katika kufanikisha maandalizi ya mkutano wake wa mwaka.
Rais
wa chama hicho ambaye anamaliza muda wake Dk. Fauz Twaib amesema wamefurahishwa
na msaada na ushirikiano uliopata chama chake kutoka Serikali katika kufanikisha
mkutano huo.
No comments:
Post a Comment