Na Hassan Hamad, OMKR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuongeza ushirikiano kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Zanzibar, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani, alipokuwa na mazungumzo na balozi mdogo wa Oman aliyefika kwa ajili ya kujitambulisha.
Amesema mabalozi waliopita wamefanya kazi nzuri kutokana na mashirikiano waliyopewa na serikali, na kwamba hatua hiyo imekuza mashirikiano katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Maalim Seif ameishukuru serikali ya Oman kwa dhamira yake ya kutoa nafasi za masomo kwa Zanzibar kupitia mfuko wa Sultan Qaboos, dhamira ambayo imeanza kutekelezwa.
Amesema hatua hiyo itaisaidia Zanzibar kuondokana na upungufu wa wataalamu katika fani mbali mbali baada ya wanafunzi wengi kuhitimu elimu ya juu chini ya ufadhili wa Serikali ya Oman.
Nae Balozi mdogo wa Oman ambaye ameanza kazi hivi karibuni Sheikh Saleh Salum, amekiri kuwa Mfuko wa Sultan Qaboos tayari umeanza kupokea maombi kadhaa kutoka Zanzibar kupitia Chuo Kikuu cha Taifa SUZA, na unaendelea kuyafanyia kazi.
Ameelezea kuridhishwa kwake na utamaduni wa Zanzibar ambao kwa kiasi kikubwa unalingana na ule wa Oman, hasa katika mavazi na sherehe za Eid.
No comments:
Post a Comment