Habari za Punde

Warioba Zungumzeni Rasimu, Sio Tume na Watu.

Na Mwandishi wetu, Dar
TUME ya Mabadiliko ya Katiba imetoa ufafanuzi kuhusu kauli mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa, imekuwa ikiingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni kuhusu katiba mpya katika mikutano ya mabaraza ya katiba ya wilaya iliyomalizika hivi karibuni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba alisema siku zote Tume yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kuwataka wanasiasa hao kujadili rasimu iliyotolewa badala ya Tume au wajumbe wake.

“Moja ya kazi za kisheria za Tume ni kutoa elimu kwa umma, na ni kazi ya wakati wote,” alisema Jaji Warioba wakati akijibu swali la waandishi waliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam kutaka ufafanuzi wa kauli ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo.

Bulembo alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akiwa mkoani Tanga akisema Tume ya Warioba imeacha kutekeleza majukumu yake na kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.

Kwa mujibu wa Tume, katika mikutano ya mabaraza ya katiba ya wilaya, wajumbe wa mabaraza hayo walikuwa na fursa ya kuuliza maswali na wajumbe wa Tume walitoa elimu kuhusu hoja na maswali yaliyoulizwa kwa mujibu wa sheria.

“Sasa anaona (Bulembo) kuwa kutoa elimu ni dhambi,” alisema Mwenyekiti huyo ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali na Waziri Mkuu.

Jaji Warioba pia alikumbusha kuwa Tume yake inafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kauli za wanasiasa na kuongeza kuwa, pamoja na kauli hizo, Tume inafarijika na kauli za kutia moyo wanazozipata kutoka kwa wananchi wa kawaida.

“Nilisema mwishoni mwa mwezi uliopita, wanasiasa wamekuwa wakitoa matamshi yaliyoifanya kazi ya Tume kuwa ngumu katika mikutano ya mabaraza ya katiba,” alisema na kuongeza.

“Matamshi mengine yalilenga Tume na wakati mwingine yalinilenga mimi binafsi au wajumbe wa Tume badala ya kuzungumzia rasimu,” alisema Mwenyekiti huyo anayeongoza Tume ya mabadiliko ya katiba yenye wajumbe 32.

Alisema Tume yake siku zote imekubali kukosolewa kwa kuamini kuwa kukosolewa ni jambo la kawaida lakini akaongeza kuwa ni vyema wananchi na wanasiasa wakajadili rasimu ya katiba iliyotolewa badala ya watu au Tume.

“Nadhani wangezungumzia rasimu wangetusaidia sana, badala ya kuzungumzia Tume na watu,” alisema Jaji Warioba na kuongeza kuwa haamini kuwa kauli za viongozi hao wa kisiasa ndiyo misimamo ya vyama vyao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.