Na Othman Ame USA.
Imeelezwa kwamba ipo haja kwa Taasisi,
Makampuni na hata Watu binafsi kuanza kufikiria kujenga nyumba kwa kuziuza kwa
bei nafuu au kutoa mkopo ili kuzisaidia jamii kuondokana na matatizo ya makazi.
Ushauri huo umetolewa na Ofisa Mkuu wa
Taasisi ya Mtandao wa ushirikiano ya Latin America { Shumake Global Partiners }
Bwana Robert Shumake wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif ambae yuko ziarani Nchini Marekani hapo katika Hoteli ya Kimataifa
ya Marriott Mjini Seattle – Washington.
Bwana Robert Shumake ambaye aliwahi kuwa
Bingwa wa mbio za Magari Duniani tayari ameshakubali kuingia ubia na Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } katika mpango wake wa ujenzi wa nyumba za
Mkopo nafuu katika eneo la Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar .
Mwanambio za Magari huyo wa Kimataifa
alimueleza Balozi Seif kwamba bado ipo idadi kubwa ya Jamii katika Mataifa
mbali mbali ulimwenguni imekosa makazi ya kudumu hali ambayo inawapa wakati
mgumu katika maisha yao
ya kila siku.
Alieleza kwamba baadhi ya watu waliokosa
makazi wamekuwa wakikumbwa na madhara mbali mbali na wakati mwengine hufikia
kufariki dunia kutokana na kukumbwa na baridi kali.
Bwana Robert Shamake alifahamisha kwamba
Taasisi yake imelenga kusaidia huduma za jamii kama
Nyumba, Afya pamoja na Sekta ya Elimu katika Mataifa tofauti ulimwenguni.
Alisema kwa kuwa tayari ameshaanza
mazungumzo ya awali na Uongozi wa ngazi ya Juu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
Zanzibar Mjini Seattle
kuhusiana na mpango huo wa ujenzi wa nyumba nakusudia kuitembelea Zanzibar Mwishoni
mwa mwezi wa Disemba mwaka huu ili kujionea hali halisi ya mazingira ya Zanzibar.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Taasisi hiyo ya Mtandao wa
ushirikiano ya Latin America kwa uamuzi wake iliyochukuwa ambao utasaidia
kustawisha jamii ndani ya Visiwa vya Zanzibar .
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ilianzisha mradi wa ujenzi wa
nyumba za maendeleo katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba ili kuwapatia wananchi wake makazi bora.
Alisema mpango huo muhimu wa serikali hivi
sasa unastahiki kuungwa
mkono na taasisi tofauti kwa vile nguvu za kuendeleza mpango huo ambao
unahitajika zaidi na jamii zimepunguwa kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya
watu Zanzibar .

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
No comments:
Post a Comment