Na Othman Ame USA
Jamii popote pale Duniani inaweza kuendelea kuishi kwa
amani, furaha na afya iwapo Wananchi wenyewe kwa kuzishirikisha Taasisi na
mashirika yaliyowazunguuka watazingatia zaidi umuhimu wa taaluma ya kinga
badala ya kusubiri tiba.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa
kitengo cha huduma za Afya cha Kampuni ya Kimataifa ya mitandao ya Mawasiliano
ya Kompyuta ya Microsoft Bwana Bill Crounse wakati akizungumza na Ujumbe wa
Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
ambao uko Nchini Marekani kwa ziara ya wiki moja ya Kiserikali.
Bwana Crounse alisema kwamba jamii kadhaa
Duniani hasa katika Nchi zinazoendelea nyingi zikiwamo ndani ya Bara la Afrika
zimekuwa zikikabiliwa na magonjwa mbali mbali yanayoibuka kila siku kwa kukosa
elimu ya kinga.
Alisema Kampuni ya Microsoft licha ya
shughuli zake za kibiashara lakini hivi sasa imeamua kutoa elimu ya kinga
katika mataifa mbali Duniani kwa lengo la kupunguza maradhi yanayosababisha
vifo ambavyo baadhi yake vinaweza kuwepukia.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa kitengo cha huduma
za kinga ya Afya cha
Microsoft alieleza kwamba Taasisi
hiyo katika kukabiliana na wimbi la maradhi imejitolea kutoka elimu ya kinga ya
afya kwa kupitia mitandao
ya mawasiliano ya kompyuta.
Bwana Bill Crounse alifahamisha kuwa
mpango huo tayari umeshahusisha zaidi ya Mataifa 120 Barari Asia na Afrika
akizitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni pamoja na Kenya, Somalia, Msumbiji,Misri
na Morocco kwa Afrika na India na Bangladesha kwa Asia.
Akizungumzia taaluma inayotolewa maskulini
na Kampuni hiyo Mkurugenzi wa
Afrika wa Microsoft Bwana Louis Onyango Otieno alimueleza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake kuwa Taasisi hiyo tayari
imeshafungua milango ya kutoa taaluma Barani Afrika kwa kutumia njia ya
mitandao.
Bwana Otieno alisema elimu hiyo
inayokadiriwa kufikia zaidi ya asilimia 44% imelenga kutolewa kwa watoto wenye umri wa miaka 15 ili
kuwajengea uwezo wa kitaaluma.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu
Zanzibar Nd. Abdulla Mzee Abdulla aliiomba Kampuni ya Microsoft kuangalia upya
mikataba iliyowahi kutiliana saini na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuendelea kusaidia sekta ya elimu Zanzibar.
Nd. Abdulla alisema Serikali ya Marekani
kupitia Taasisi zake ikiwemo ile ya Microsoft ziliwahi kusaidia kuanzisha mradi
wa kuimarisha elimu kwa kutumia mitandao ya kompyuta kwa skuli za msingi Unguja
na Pemba.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Kampuni hiyo ya Microsoft kwa juhudi
zake inazochukuwa za kusaidia taaluma tofauti ikilenga zaidi zile nchi
zinazoendelea ikiwemo Zanzibar.
Balozi Seif alisema misaada ya taasisi
hiyo kwa kiasi kikubwa imeziwezesha nchi changa kupiga hatua kubwa kielimu na
kuiomba Kampuni hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za
kuimarisha sekta ya elimu.
Baadaye Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake waliendelea na ziara yao
kwa kutembelea Ofisi za Mfuko wa Kimataifa wa misaada wa Bill na Melinda Gates
zilizopo kati kati ya mji wa Seattle - Washington.
Katika mazungumzo yao Ofisa Mipango wa
Mfuko huo Bibi Windy Wilkins alisema Taasisi hiyo inajaribu kuangalia uwezekano
wa namna ya kuisaidia Zanzibar katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu.
Bibi Windy alisema hivi sasa taasisi hiyo
kupitia mpango wa AGRA imepanga kuongeza nguvu katika utoaji wa taaluma ya
uzalishaji wa maziwa na vifaranga ikilenga kuwajengea zaidi uwezo wafugaji wadogo wadogo.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana
na wafugaji wengi kuishi vijijini kiasi kwamba taaluma ndio njia pekee
itakayowawezesha kuingia katika soko la kimataifa litakalowapa nguvu na uwezo
wa kuongeza kipato chao.
“ Kwa kutambua kuwa kilimo ni gari ya
Biashara Taasisi yetu imeamua kujipangia kutumia Dola za Kimarekani Milioni mia
Nne kwa mwaka katika miradi ya Taaluma “. Alifafanua Bibi Windy Wilkins.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliueleza Uongozi wa Mfuko wa Misaada wa Kimataifa
wa Bill na Melinda Gates kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla muda wote imekuwa ikitilia mkazo
sekta ya Kilimo ambayo ndio uti wa mgongo wa Taifa.
Balozi Seif alisema wananchi wengi wa
Tanzania na Zanzibar wamekuwa wakiishi katika maeneo ya mashambani kwa zaidi ya
asilimia 80% idadi ambayo inapaswa kusaidiwa kitaaluma ili izalishe kitaalamu
zaidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliuomba Uongozi wa Mfuko wa Kimataifa wa Misaada wa Bill na Melinda Gates
kutuma Timu ya wataalamu wa sekta ya kilimo kutembelea Zanzibar ili kuangalia
maeneo ambayo wanaweza kusaidia.
No comments:
Post a Comment