Toronto,
Canada
November 03,
2013,
Jumuiya ya
Diaspora ya Canada, Zanzibar-Canadian Diaspora Association-ZACADIA, ambayo
inajulikana rasmi kwa jina la ZACADIA Foundation, juzi November 02, 2013,
iliandaa hafla ndogo ya kutunisha mfuko wa kuwasaidia watoto mayatima ambao
wamo katika mpango wa mradi maalum wa kuwadhamini watoto hao unaojulikana kwa
jina la Zanzibar Children Funds Program.
Hafla hiyo
ambayo ilifanyika katika ukumbi wa kijamii wa
“Lawrence Heights Community Centre” ilianza kwa kusomwa risala ambayo imeelezea
historia ya ZACADIA na kazi ilizozifanya na mafanikio yaliyofikiwa.
Baada ya
risala hiyo, Imam Abdufataah alisimama na kusoma dua ya ufunguzi na baadaye
kusimama Maalim Ali kwa kutoa hotuba ya kuhamasisha waliohudhuria na wale wasiokuwapo
katika kusaidia mayatima.
Katika
hotuba yake, alisema kwamba zamani ilikuwa hakuna suala la watoto mayatima kuchangiwa kwa sababu kila mmoja miongoni mwa
jamii alikuwa akifanya wajibu wake licha ya kuwa hali zao za kiuchumi zilikuwa
ni duni kulinganisha na sasa hivi, ambapo watu wengi wana uwezo, lakini
wanashindwa kujua nani ameamka salama na ameshinda vipi, amekula nini na
anavaa vipi.
“Siyo kwamba zamani kulikuwa hakuna mayatima visiwani kwetu,
lakini ilikuwa hukuti kuwaona watu wanawachangia mayatima hao misikitini au
katika mihadhara kama hii, kwa sababu kila mmoja alikuwa anamjali mwenzake.
Kabla mtu hajatoka kwenda na shughuli zake, alikuwa akihakikisha kuwa jirani
yake ameamka salama na kama kuna mtu ana yatima au mayatima, basi alikuwa akihakikisha
familia hiyo hailali na njaa waka kutembea na matambara mwilini. Laiti kila
mmoja wetu angalifanya wajibu wake kama tunavyoelezwa na dini yetu, basi
mihadhara kama hii ya kuwaombea mayatima isingalikuwapo,” alimalizia maalim
Ali.
Katika
hafla hiyo, pia ilioneshwa PowerPoint ya mradi wa watoto mayatima ambao umeanza
kufanyiwa kazi. Pia ilioneshwa PowerPoint ya mradi wa Wazee na Wanawake ambapo
msimamizi wa Idara hiyo aliwasili Zanzibar hivi karibuni na kutoa misaada ya vitu
mbali mbali kwa wananchi wanaohitaji Unguja na Pemba.
Hafla kama
hii inategemewa kufanyika tena katika mwezi wa December mwaka huu katika ukumbi
wa Driftwood Community Center ambapo ni kitovu cha eneo wanaloishi Wazanzibari
wengi katika GTA.
Jumla ya
dola 125 za Canada zilikusanywa katika hafla hiyo. Baadhi ya waliohudhuria
walichukuwa fomu za kuahidi kuchangia kidogo kidogo kwa mwaka. Pia kulifanyika
mnada mdogo wa picha za Msahafu na msahafu mmoja wa herufi kubwa ambao vitu
hivyo vyote vilitolewa sadaka na wana Diaspora waliohudhuria.
Pia mtoto mmoja
miongoni mwa watoto mayatima waliomo katika mradi huo alipata mdhamini wa
kumshughulikia kama mwanawe kwa huduma za elimu, afya, nguo, chakula na huduma
nyengine hadi atakapomaliza sekondari na baadaye ZACADIA kujaribu kumtafutia scholarship
kwa ajili ya masomo ya juu.
Mtoto huyo ambaye anatokea sehemu za Kiungoni huko
Kaskazini, Pemba ni Fatma M. Saleh
No comments:
Post a Comment