Habari za Punde

Nyumba 14 Shumba Mjini zaungua moto

 Moja kati ya nyumba 14 katika Kijiji cha Shumba Mjini Wilaya ya Micheweni ziliztoathirika kwa moto mkubwa ulitokea majira ya saa 5.00 asubuhi ya jumapili huku wakaazi wake wakichanganyikiwa kutokana na maafa hayo.

 Baadhi ya wananchi 100 ambao nyumba zao 14 zimeathirika na vibaya na moto katika Kijiji cha Shumba Mjini wakipata hifadhi kwenye madrasa moja Kijijini hapo.

 Moja kati ya nyumba 14 zilizoathirika na moto katika kijiji cha Shumba Mjini ambapo wakaazi wake wakiwa wamechanganyikiwa kutokana na janga hilo.

 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Shehani Mohd Shehani akitoa tathmini ya awali ya uchunguzi wa moto uliotokea Shumba Mjini mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Sei aliyefika kijijini hapo kuwapa pole wananchi walioathirika na maafa hayo.

Kulia ya Balozi Seif ni Mwakilishi wa Jimbo la Micheweni Mh. Subeit Juma Khamis na kushotoni kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini pemba Mh. Dadi Faki Dadi na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Kanal Mstaafu Juma Kassim Tindwa.
Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ. 
 
 
Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Pemba kufanya tathmini mara moja nyumba zote zilizoathirika kutokana na moto mkubwa uliokikumba Kijiji cha Shumba Mjini leo majira ya saa 5.00 za asubuhi.
 
Nyumba zipatazo 14 zikiwa na wakaazi 100 zimeathirika vibaya kutokana na moto huo na nyengine  24 kuezuliwa mapaa yake kwa hofu ya kuathirika na moto huo ambao hadi sasa kwa mujibu wa taarifa za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Shehani  Mohd Shehani kwamba chanzo chake bado hakijafahamika huku uchunguzi wa jeshi la polisi pamoja na vikosi vyengine vya ulnzi ukiendelea.
 
Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar akiwa kisiwani Pemba kwa shughuli mbali mbali za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar alitoa agizo hilo muda mfupi baada ya kuwafariji  wananchi wa Kijiji cha Shumba Mjini kutokana na maafa waliyoyapata ya janga la moto.
 
Akiwapa pole wananchi hao 100 waliohifadhiwa kwenye madrasa mmoja Kijijini humo na baadaye kupelekwa Skuli ya Kijiji hicho Balozi Seif aliwataka kuwa na subra katika kipindi hichi cha mitihani na Serikali inajipanga kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi hao.
 
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaandaa kikao maalum cha dharura keshokutwa jumatatu ili kulijadili suala hili na kuona jinsi itakavyoweza kukusanya nguvu za kuwasaidia wananchi walioathirika na janga hili.
“ Wakati nimeshamuagiza Mkuu wenu wa Mkoa kufanya tathmini ya janga hili mimi kama mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na vile vile nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar nitawajibika kuitisha kikao cha dharuura Jumatatu kulitafakari suala  hilo  “. Alisema Balozi Seif.
 
Alisisitiza kwamba ni wajibu wa Serikali Kuu kutafuta mbinu na utaratibu utakaoweza kutoa fursa nzuri ya kujaribu kusaidiana Wananchi walioathirika na Maafa hayo.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru wananachi na baadhi ya Taasisi zilizojitokeza kwa njia mbali mbali kusaidia wananchi hao ikiwemo vyakula, vifaa na baadhi ya huduma muhimu kama nguo kwa wale wananchi 100  waliokuwa wakiishi kwenye zile nyumba 14 zilizounguwa na kuteketeza vitu mbali mbali.
 
Aidha Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Wilaya ya Micheweni pamoja na Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa hatua iliyochukuwa ya kuandaa mazingira ya kuwahifadhi  wale wananachi watakaokosa hifadhi na kuwapeleka katika Skuli ya Kijiji hicho cha Shumba Mjini.
 
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wananci wa Kijiji cha Shumba Mjini Mwakilishi wa Jimbo la Micheweni Mh. Subeit Juma Khamis amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa hatua aliyochukuwa ya kuwafariji wananchi hao katika muda mfupi baada ya kutokea tukio hilo.
 
Mh. Subeit alimuelezea Balozi Seif kuwa ni kiongozi mwenye moyo unaomuelekeza kujali wananchi wake.
 
Moto huo mkubwa uliokuwa ukivuma kutokana na upepo mkali licha ya taarifa za awali za kutotambulikana chanzo chake ulianzia kwenye Nyumba ya Bwana Masoud Ali Khamis na baadhi ya wananchi walisikika wakisema chanzo chake kimesababishwa na watoto waliokuwa wakijiandaa kupika mlo wa mchana.
 
 
 
 
 

3 comments:

  1. Tukio limetokea jana asubuhi, basi Zanzinews wameshindwa kuripoti jana yote? Au halina umuhimu huo bali yenye umuhimu ni mabanda ya Beit al Ras.
    Wakati Serikali inatafakari, waziri anaeshughulika na vikosi vya SMZ akae chonjo kwani hana uwezo au ni mvivu wa kufikiri. Hakuhitajiki science ya kurusha roketi kwamba Wilayani kuwe na angalau gari moja la kuzima moto.

    ReplyDelete
  2. @Ibn abdullaziz,

    Mbona tukio hili lilikuwepo kwenye Face book jana na lilitolewa na Bi salma Saidi, mimi nililisoma kutoka huko. na yeye nafikiri alilitoa kutoka kwa Zanzinews..Isipokua picha tu Zanzinews walikua hawajaziweka..

    Hata hivyo magazeti yetu ya Serikali tusitegemee mengi wao ni kama Makasuku kwani wanaogopa ku-critisize SMZ na uongozi wa Government... Mimi hujiuliza ivo kweli tutafika kwa waandishi hawa wasiojua nini maana ya Uandishi... Kwa mfano hao Zanzinews wakitoa picha ni kusifu SMZ na serikali tu au kutoa matokeo ya Kijamii.. Lakinio hakuna hata pamoja wanapokosoa Serikali...

    Kunakazi kubwa yakufikia democrasia ya kweli visiwani, ikiwa magazeti wameshaitwa na raisi na kutishwa kufungiwa magazeti yao kama wataripoti kinyume na SMZ CCM wanavyotaka... Si umeona TVZ inavoonyesha Mikutano ya Wahafidhuna wa UVCCM wanavoendelea kuwatukana Viongozi wenye asili ya Pemba....
    Hiyo ndio Faida ya Mapinduzi.... na hao akina Zanzinews Salma saidi ndio watoto wa kimapinduzi... tuwapigie makofi kwakutuletea Picha za nyumba na habari Bubu... Wanachunga Unga wao... Ni lazima kuwe na Jounalist mmoja ambae anajua sheria na haki yake ya kuripoti mambo yaliokua mazuri na mabaya.. we need a break through.. may be others would be follow a good examples.

    ReplyDelete
  3. Mimi nafikiri serikali haioni umuhimu wa watu wa pemba kweli wanashindwa kuweka faya wilaya tatu mkoani wete na micheweni kazi yao kuvimba matumbo na kuwakamua wapemba kwa uchumi wao wa karafuu .

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.