Habari za Punde

ZECO kupandisha tena bei ya umeme

Na Mwandishi wetu
SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO) litapandisha tena bei ya umeme baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuliruhusu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuongeza bei ya umeme.
Akizungumza na kituo cha redio cha Zenj FM jana, Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar, Nd. Hassan Ali Mbarouk, alisema taratibu za kuongeza bei ya umeme zinafanywa, ingawa alisema bado hajafahamu malipo hayo mapya yataanza lini.
Alisema kwa sasa wateja wa Shirika hilo wataendelea kulipa bei ya sasa wakati shirika likiendelea na utaratibu wa kuweka bei mpya.
Bei hiyo mpya inakuja wakati ni hivi karibuni tu shirika hilo lilipandisha gharama za huduma za umeme, ambazo hata hivyo bado zinalalamikiwa na wateja.
 Alisema bei hiyo mpya, inaweza kuwashtua wateja, lakini alisema ndio hali ya biashara na kwamba ZECO haina jinsi zaidi ya kuridhia mabadiliko hayo.
Aliwataka wateja kutumia umeme kwa uangalifu ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi wa EWURA, Nd. Felix Ngamlagosi,alitangaza rasmi ongezeko la gharama za umeme kwa asilimia 50 gharama ambazo zilianza kutumika rasmi Januari Mosi 2014.
Alisema Oktoba 11, mwaka jana TANESCO liliwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Ewura na kupendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia Oktoba 1, jana.
 Alisema Tanesco pia iliomba ongezeko la asilimia 12.74 kuanzia Januari 1, 2014 na asilimia 9.17 kuanzia Januari 1, 2015.
Hali hiyo imefanya kundi la wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa juu, likiwamo Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco), umeme umepanda kwa shilingi 53, kutoka shilingi 106 hadi shilingi 159 kwa uniti moja sawa na ongezeko la asilimia 50.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,Felchesmi Mramba, alisema TANESCO inazidai taasisi za serikali kiasi cha shilingi  bilioni 129 kati ya hizo shilingi bilioni 70 ni deni la Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.