Habari za Punde

USAID yagawa baiskeli 123 kusaidia huduma za wajawazito,watoto

Na Asya Hassan
SHIRIKA la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID), limekabidhi baiskeli 123 na vifaa vya kufundishia kwa wahudumu wa afya ya jamii wa Zanzibar ili ziweze kuwasaidia katika harakati zao za kutoa huduma hiyo kwa mama wajawazito na watoto.

Hafla hiyo iliyofanyika kituo cha afya Dunga wilaya ya kati Unguja, ambapo Mwakilishi wa Mkurugenzi wa USAID Tanzania, Erick Mlanga na Mkurugenzi Mkazi wa Jhpiego nchini Tanzania, Maryjane Lacoste walimkabidhi vifaa hivyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Mohammed Saleh Jidawi.

Katika makabidhiano hayo, Dk. Jidawi, alisema juhudi zinazofanywa na Wizara ya Afya Zanzibar kwa kushirikiana na USAID zina lengo la kuhakikisha Zanzibar inafikia lengo la millennia la  kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto.

Alisema mradi huo umeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwaelimisha mama wajawazito kwenda kuzalia hospitali na vituo vya afya na kuacha tabia ya kuzalia majumbani.


Hata hivyo, alisema baskeli na vifaa walivyokabidhiwa wahudumu wa afya ya jamii zitawarahisishia katika kazi zao pale wanapokwenda kutoa huduma.

Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru USAID na Jhpiego kwa kuuwezesha mradi huo muhimu kwa maendeleo ya wanawake na watoto.

 Nae Mwakilishi wa Mkurugenzi wa USAID Tanzania, Erick Mlanga, alisema mradi huo umewawezesha wanawake wengi kuwasaidia wanawake wezao ili kujifungua katika mazingira salama.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Jhpiego nchi Tanzania, Maryjane Lacoste, alisema kuanzia mwaka 2008 watu wa Marekani kupitia mradi wa MAISHA wamekuwa wakishirikiana na Serikali ya Zanzibar katika kuboresha afya ya mama na mtoto katika vituo tisa vya afya Unguja na Pemba.

Nae Mratibu wa afya ya uzazi ya mama na mtoto wilaya ya kati Unguja, Mwanamvua Mussa, alisema katika shehia sita zilizomo kwenye, kulikuwa na maendeleo kwa wanawake kujhifungulia vituo vya afya.


Kati ya baiskeli hizo,72 zitagaiwa kwa wahudumu wa afya ya jamii wilaya ya Wete, Mkoani na Micheweni Pemba na baiskeli 51 kwa wahudumu  wa afya ya jamii wilaya ya kati na kaskazini 'A'.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.