Habari za Punde

Dk Shein aishauri Wizara ya Mifugo na uvuvi kuanzisha Chuo cha uvuvi

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                     24 Aprili , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema wakati umefika kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanza kufikiria uwezekano wa kuanzisha chuo cha Uvuvi Zanzibar.
 
Dk. Shein amesema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na uongozi wa Wizara hiyo katika mkutano wa kujadili Mpangokazi na bajeti ya mwaka 2013/14 ya Wizara hiyo kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia mwezi Julai 2013 hadi Machi 2014 uliofanyika  Ikulu mjini Zanzibar.
 
Amesema mazingira ya kisiwa cha Zanzibar, mahitaji ya ajira kwa vijana na azma ya serikali ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa samaki, vinalazimisha kuweko kwa chuo maalum cha uvuvi kitakachosaidia kutoa  mafunzo kwa wananchi wa Zanzibar wanaojihusisha na shughuli za uvuvi na hasa vijana.
 
Vile vile Rais wa Zanzibar amesisitiza haja ya viongozi na wafanyakazi wa taasisi za umma kuandika taarifa za ziara za kimafunzo wanazohudhuria ndani na nje ya nchi na kuzifanyia kazi taarifa hizo ili ziweze kuwajengea uwezo wafanyakazi wengine ambao hawakupata fursa hizo.
 
“tija ya ziara zinazofanywa na watumishi wa umma katika sehemu mbali mbali ndani na nje ya nchi inaweza kupatikana iwapo tu wanaofanya ziara hizo wataandika taarifa kuhusiana na wanayojifunza kutokana na ziara hizo na kuwataarifu wengine wasiopata fursa hizo’ alisema Dk. Shein.
 
Akizungumzia umuhimu wa kuwa na mipango mizuri ya serikali, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameitaka Wizara hiyo kuhakikisha kuwa inakuwa na mipango mizuri itakayoweza kutekelezeka kwa ufanisi.
Amesema mipango mizuri ya serikali ni ile itakayopangwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya watendaji wote kwenye taasisi husika.
 

Aidha, amesema ni vyema taasisi zote za umma zikazingatia thamani halisi ya bei ya bidhaa na huduma zitakazohitajika wakati wa kupanga na kutekeleza majukumu ya taasisi zao ili kuwa na bajeti halisi kwa mahitaji halisi.
 
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Wizara yake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Kassim Gharib Juma amesema Wizara yake imekuwa ikipata mafanikio makubwa katika sekta ya mifugo na uvuvi katika kipindi cha mwaka 2013/14.
 
Aliyataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa maziwa kutoka tani 24,343 mwaka 2012 hadi tani 27,244 mwaka 2013 ikiwa ni ongezeko la asilimia kumi na moja, uzalishaji wa mayai umeongezeka kutoka tani 105, 125 mwaka 2012 hadi kufikia tani 130,464 mwaka 2013 ambalo ni ongezeko la asilimia 19 huku nyama ya ng’ombe katika kipindi hicho imeongeeka kwa asilimia 17.
 
Katika taarifa yake hiyo Dk. Gharib alieleza pia kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika udhibiti wa maradhi yasiyo na mipaka pamoja na maradhi ya kichaa cha mbwa kutokana na kuimarika kwa huduma za chanjo.
 
Kwa upande wa sekta ya uvuvi, Dk.  Kassim amesema kumekuwa na ongezeko la uvuvi wa baharini na pia wananchi wengi wameshajiika kuendeleza ufugaji wa samaki na mazao ya baharini.
 
Alibainisha kuwa jumla ya tani 23,000 za samaki zilivuliwa  kwa kipindi cha miezi tisa kwa mwaka wa fedha 2013 – 2014 ambazo zimewaingizia wavuvi  jumla ya shilingi bilioni 89.7.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.