Na Mwandishi wetu, Dar
es Salaam
KILELE cha sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ‘nusu karne’
ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar zilizofanyika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam jana
zimefana na kuwa za aina yake.
Uwanja huo ulipambwa kwa mapambo mbalimbali ikiwemo picha
za viongozi, Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapnduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, bendera za Taifa, pamoja na maumbo mbalimbali
yaliyokuwa yakifanywa na vijana wa halaiki, ambao walikuwa kivutio kikubwa kwa
hadhira, huku rangi za bendera za mataifa tafauti ambayo yalihudhuria sherehe
hizo zikipamba sherehe hizo.
Aidha nembo maalum ya sherehe hizo ambayo ina picha za
waasisi wa Muungano, marehemu mwalimu Julius Kambarage Nyerere na marehemu mzee
Abeid Amani Karume, zilienezwa uwanja mzima na kugaiwa kwa wananchi wote
walioingia uwanjani, ambao pia walipewa bendera za Taifa.
Mgeni rasmi katika sherehe hizo, ambae pia ndie mwenyeji,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliingia uwanjani
saa nne na nusu asubuhi kwa gari la wazi
akiongozwa na mapikipiki ya askari trafiki waliopambwa kwa mavazi meupe,
alizunguka uwanja mzima kusalimiana na wananchi ambao nao walimpongeza kwa
shangwe kubwa.
Baada ya kumaliza mzunguko wa kusalimia wananchi, Rais
Kikwete alipigiwa wimbo wa Taifa, pamoja na mizinga 21 salama kwa heshima yake
kabla ya kukagua gwaride rasmi la vikosi vya ulinzi na usalama.
Baadae vikosi vya ulinzi na usalama vilipitia mbele ya Rais
kutoa heshima kwa mwendo wa pole na baadae vikaingia vikosi vilivyopita kwa
mwendo wa kasi na kuonesha ukakamavu wa kijeshi.
Pia kwa upande wa Tanzania walikuwepo Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda na Mawaziri na watendaji wengine wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Viongozi wengine wa Zanzibar walioshiriki sherehe hizo ni
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, pamoja na Mawaziri na watendaji wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi kutoka mikoa yote mitano ya
Zanzibar.
Wake wa viongozi wa kitaifa wakiongozwa na mke wa Rais mama
Salma Kikwete, pamoja na wake wa waasisi wa muungano mama Fatma Karume na mama
Maria Nyerere nao walishiriki hafla hiyo kubwa na ya aina yake.
Onesho la mbwa wa polisi waliofunzwa kupambana na ghasia
nalo lilikuwa kivutio, pamoja na ukakamavu uliooneshwa na askari wa magereza
katika kukabiliana na ghasia zitapotokezea katika magereza.
Miongoni mwa vivutio vikubwa na vya kipekee ni wanajeshi wa
miemvuli ambao walitua uwanjani baada ya kutoka katika ndege zilizopita
uwanjani hapo ikiwa katika urefu wa futi 4500 kutoka usawa wa bahari, wakiwa na
silaha pamoja na bendera ya taifa, jambo ambalo ni jipya kwa wengi wa hadhira
hiyo ambao wamekuwa wakiona mambo hayo kupitia michezo ya televisheni na
sinema.
Katika kuonesha mvuto wa askari hao wa miemvuli, Rais
Kikwete aliwapa heshima maalum ya kupanda jukwaani na kusalimiana nao kwa
kuwapa mikono.
Makomandoo nao walionesha uwezo wao wa kupambana na adui
kwa kutumia mikono kama ndio silaha pekee,
jambo ambalo lilifurahiwa na kuwavutia wengi, wakiwemo viongozi na wananchi.
Vifaa vya kijeshi vikiwemo vya kivita kama
ndege za kivita ambazo zilipita chinichini, pamoja na vifaru, mizinga na magari
mengine ya kivita navyo vilikuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya sherehe hizo.
Miongoni mwa wageni mashuhuri walioshiriki sherehe hizo ni
Mfalme Mswati wa tatu wa Swaziland, Rais Joyce Banda wa Malawi, Rais Uhuru
Kenyata wa Kenya na Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Makamu wa Rais wa Zambia,
waziri wa Serikali za mitaa, Bernito De Souza. Makamu Mwenyekiti, Umoja wa
Afrika, Erastus Mwencha.
Pia alikuwepo Mfalme wa Lesotho, Majest Letsie III, Waziri
Mkuu wa Rwanda, Pierre Habumuremyi, Waziri Mkuu wa Msumbiji, Mentho Anthonio, Waziri Mkuu wa Misri na
Makamu wa Rais wa Nigeria, Mohammed Namad.
Wengine ni kutoka Oman, Dk. Rawiya Al-Busaidy waziri wa
Elimu ya Juu, Waziri wa Angola, Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Said Hassan,
kutoka Ushelisheli, waziri Tibeto, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Tedros
Adhanom, Waziri wa Mawasiliano wa Algeria, Abdelqadir Messahel, Mabalozi Maalum
kutoka Ghana, Kingsley Saka Abdulkarim na kutoka Eritrea.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge la China ,
Chen Chanqin nae alihudhuria kilele hicho, ikizingatiwa kuwa sherehe hizo
zinakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya mahusiano kati ya China na Tanzania .
Viongozi wengine wa Mashirika ya kimataifa walioshiriki ni
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Balozi wa Ufaransa,
Balozi wa Korea Kusini, Brazil Balozi wao.
Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania , walihudhuria sherehe hizo na
kuiwezesha dunia nzima kukutana katika maadhimisho hayo, hali inayoashiria
mahusiano mema kati ya Tanzania
na dunia.
Marais wastaafu waliohudhuria sherehe hizo ni Benjamin
Mkapa, Dk. Amani Abeid Karume, Mwai Kibaki wa Kenya
na Dk.Sam Nujoma wa Namibia .
Wanafunzi 3547 kutoka skuli za Tanzania Bara na Zanzibar walifanya
maoneso mbalimbali ya halaiki ambayo yalionesha maumbo ya tokea kuasisiwa kwa
muungano huo na mafanikio yaliyopatikana ambapo hadhira ilipata burudani ya
kutosha na kufurahia umahiri wa watoto hao.
Muungano wa Tanzania umeendelea kuwa wa kipekee
ulimwenguni kutokana na ukweli kwamba, nchi nyingi za Afrika ziliungana lakini
hazikuweza kudumu kwa muda mrefu ikiwemo, Ghana, Guinea na Mali ziliungana
lakini muungano wao ulivunjika baada ya miaka michache na kila nchi kurudi
kivyake, Senegambia imevunjika na kurudi Senegal na Gambia, Ethiopia na
Eritrea, Somalia na Sudan. Mwengine ni ule wa Ethiopia
na Eritrea ambao baadae
ulivunjika na kuzusha vita baina yao
na uhasama unaoendelea hadi leo.
Huko Ulaya kuna nchi kama Czchekoslovakia ambazo sasa
zimeachana na kuwa Jamhuri ya Czech na Slovakia ,
Shirikisho la Sovieti ambalo limesambaratika likiwa na nchi nyingi, Ujerumani
ambayo hata hivyo imeungana tena hivi sasa baada ya kuwa Ujerumani Mashariki na
Ujerumani Magharibi, pamoja na Korea
ambayo sasa ni Korea
mbili ya Kusini na Kaskazini.
Uwanja wa uhuru ulishindwa kuhimili idadi ya watu
waliofika kushuhudia sherehe hizo, hivyo kulazimika baadhi ya watu kuruhusiwa
kuingia katika uwanja wa Taifa ulio pembeni na kuona sherehe hizo, huku nje ya
viwanja kukiwekwa screen maalum kwa walikosa nafasi kuingia ndani.
Akitoa salamu za shukurani, mbali ya kupongeza vikosi,
wasanii na wote waliofanikikisha sherehe hizo na wageni waliohudhuria, alisema
watanzania wana kila sababu ya kusherehekea sherehe hizo huko hotuba ya Rais
kwa sherehe hizo aliitoa juzi jioni, ambapo usiku wa juzi kulikuwa na mkesha wa
sherehe maalum za fashifashi Mjini Zanzibar.
Hata hivyo viongozi wa Mataifa mbalimbali waliohudhuria
sherehe hizo walipewa nafasi na mwenyeji wao Rais Jakaya Kikwete kutoa salamu
kwa Watanzania, ambapo wote waliipongeza Tanzania na kuiombea iendelee kuwa
na amani, umoja na utulivu katika muungano wao.
Aidha katika upekee wa sherehe hizo na kutoa nafasi kwa
wananchi wengi zaidi kushiriki, jumla ya wananchi 4000 ikiwa 2000 kutoka
Zanzibar na 2000 kutoka Bara walipita kiwanjani hapo kwa maandamano
yaliyoongozwa na farasi, pamoja na watu 50 waliozaliwa tarehe 26 Aprili na
baadae wapanda pikipiki na waendesha baskeli walipita katika maandamano hayo.
Viongozi na Makamanda wa Vikosi vya ulinzi na Usalama
waliovalia sare maalum, pamoja na wapiganaji wao nao walitoa mvuto maalum
katika sherehe hizo adhimu.
Mbali ya vikundi vya ngoma za asili kutoka Bara na Zanzibar , sherehe hizo zilipambwa kwa wimbo maalum
ulioimbwa na mchanganyiko wa wasanii wa nyimbo mbalimbali kutoka Bara na Zanzibar ambao uliwavutia
wengi.
Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar
umekuwa na mafanikio mengi kwa wananchi wao pande mbili hizo kiuchumi, kijamii
na kiusalama, ambapo pia umewekwa utaratibu maalum wa kutatua changamoto
zinazojitokeza katika muungano huo ndio maana ukadumu hadi leo.
Katika hatua za kuuimarisha muungano huo wa Tanzania , hivi
sasa inaendelea na mchakato wa kutayarisha katiba mpya ili iendane na hali
halisi na mazingira ya sasa, ikiwa ni miaka 50 tokea kuasisiwa muungano huo.
Kabla ya kilele hicho maadhimisho hayo yalishuhudia
kufanyika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na makongamano, matembezi ya
hisani, michezo ya kitaifa na kimataifa nchini kote, hali iliyoonesha muamko wa
wananchi kushiriki maadhimisho hayo.
Ukiachia sherehe hizo kutangazwa na kuoneshwa moja kwa
moja na baadhi ya vituo vya televisheni na redio hapa nchini, waandishi wa
habari wa magazeti na vyombo vyengine vya kitaifa na kimataifa, nao walikuwa
mstari wa mbele kuchukua habari na picha ili kuwafikishia wananchi kupitia
vyombo vyao, jambo lililoonesha uzalendo na uwajibikaji wa vyombo vya habari
kwa mambo ya kitaifa.
Kauli mbiu ya sherehe hizo za nusu karne ya muungano ni ‘Utanzania
wetu ni Muungano wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na kuudumisha’ ukiwa na lengo la
kuuimarisha na kuudumisha zaidi muungano huo.
No comments:
Post a Comment