Habari za Punde

Maalim Seif Arejesha Fomu.

 Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akirejesha fomu ya kugombea tena Katibu Mkuu wa Chama hicho kwa katibu wa (CUF) Wilaya ya Magharibi Bw. Juma Rajab, katika ofisi za CUF Wilaya ya Magharibi, Kilimahewa Unguja.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wafuasi wa CUF waliojitokeza wakati akirejesha fomu ya kugombea tena nafasi ya Katibu Mkuu, katika ofisi za CUF Wilaya ya Magharibi, Kilimahewa Unguja. 
 Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Magharibi Unguja akizungumza wakati Maalim Seif akirejesha fomu ya Kugombea tena nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama hicho.
 Wafuasi wa CUF wakimsikiliza Maalim Seif baada ya kurejesha fomu ya kugombea tena nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama hicho katika ofisi za CUF Wilaya ya Magharibi, Kilimahewa Unguja. (Picha na Salmin Said, OMKR)


Na Hassan Hamad
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amerejesha fomu ya kugombea tena nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama hicho, na kusisitiza msimamo wake wa kuendelea kuwaunganisha Wazanzibari.

Akikabidhi fomu hiyo kwa Katibu wa CUF Wilaya ya Magharibi Unguja Bw. Juma Rajab, Maalim Seif amesema suala la ubaguzi kamwe halitopewa nafasi ndani ya chama hicho.

Amefahamisha kuwa wazanzibar wote ni wamoja bila ya kujali asili ya mtu anapotokea ndani ya visiwa vya Zanzibar, na kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Maalim Seif amerejesha fomu hiyo baada ya kuamua kuingia tena kwenye kinyang’anyiro hicho na kuchukua fomu Ijumaa iliyopita, ambapo alisindikizwa na viongozi wa CUF na wafuasi kadhaa wa chama hicho.

Amesema CUF ni chama kinachoheshimu demokrasia, na kuwataka wanachama wanaoweza kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho kufanya hivyo bila ya woga kwani ni haki yao ya kikatiba ndani ya chama.

“Nafasi hii haina mwenyewe, kwa hivyo mwenye ubavu aingie bila ya kujali kuwa anagombea nani”, Maalim Seif aliwahamasisha wafuasi wa chama hicho.

Akizungumzia kuhusu chaguzi zinazoendelea ndani ya chama, Maalim Seif amesema zinaendelea vizuri na tayari wanaendelea na chaguzi ngazi ya Wilaya, baada ya kukamilika katika ndazi za matawi na majimbo.

Amesema hadi sasa tayari wameshafanya chaguzi katika Wilaya tano zikiwemo Wilaya zote nne za Pemba pamoja na Wilaya ya Kaskazini 
“A” Unguja, ambapo Wilaya zilizobaki za Zanzibar zinatarajia kukamilisha chaguzi zake mwishoni mwa wiki hii.

Amewataka viongozi waliochaguliwa kuwa wajasiri na kusimamia umoja na mshikamano, ili kukiwezesha chama hicho kufikia malengo yake ya kushika hatamu za uongozi wa nchi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mapema akizungumza katika hafla hiyo ya kurejesha fomu, Mkurugenzi wa haki za binadamu, habari na uenezi wa CUF Bw. Salim Bimani, amesema safari ya kukiimarisha chama hicho inaendelea, na hawatorudi nyuma hadi watakapofikia malengo yao.

Wakati wa kurejesha fomu hiyo, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisindikizwa na viongozi wa chama hicho akiwemo Naibu Katibu Mkuu Hamad Massoud Hamad, Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu na mjumbe wa kamati ya maridhiano Mansoor Yussuf Himid.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.