Habari za Punde

Ali Issa hatunaye tena

Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Ali Issa Simai Kapten (katika picha ndogo) likipelekwa mazikoni leo

Na Salum Vuai, ZANZIBAR
MCHEZAJI mstaafu wa timu ya soka ya KMKM Ali Issa Simai, amefariki dunia jana wakati wa magharibi baada ya kuugua kwa muda mfupi, na kuzikwa leo huko Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja.
Marehemu, ambaye alijulikana zaidi kwa jina la ‘Kepteni’ kutokana na kuwa nahodha wa KMKM kwa muda mrefu, alikutwa na mauti nyumbani kwake Fuoni baada ya kurudi kutoka katika shughuli zake za kawaida. 

Mwaka 1974, kiungo huyo mshambuliaji  alijiunga na timu ya kikosi cha wanamaji wakati huo ikiitwa Navy na kudumu nayo hata ilipobadilishwa jina na kuitwa KMKM (Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo), akitokea klabu ya Ujamaa yenye maskani yake mtaa wa Rahaleo.


Mmoja wa wanasoka waliocheza pamoja naye Abdalla Maulid, ameliambia gazeti hili kuwa, marehemu alikuwemo kwenye kikosi cha washika magendo hao kilichoshiriki michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1974 yaliyofanyika mjini Dar es Salaam, yakiwa katika mwaka wake wa kwanza.

Maulid alifahamisha kuwa, mwaka 1975, kepteni huyo aliitwa katika timu ya taifa ya Zanzibar iliyoshiriki mashindano ya Chalenji kwa vijana, yaliyofanyika uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, na ubingwa kuchukuliwa na Kenya.

Aidha mwaka huo wa 1975, marehemu aliyesifika kwa umahiri wake wa kumiliki mpira na mbinu za kufumania nyavu, aliteuliwa katika timu kubwa ya taifa iliyokuwa chini ya kocha Muingereza George Dunga.Pamoja na kuibeba vyema klabu yake katika ligi kuu ya muungano kuanzia mwaka 1976 na kufanikiwa kutwaa ubingwa mwaka 1984, marehemu Ali Issa pia aliisaidia Navy (sasa KMKM) kucheza klabu bingwa Afrika mwaka 1978, ambapo walifika hatua ya nne bora.

Nahodha huyo alidumu na KMKM hadi mwaka 1990 alipoamua kutundika madaluga, na kuendelea kuchezea timu ya maveterani, Wazee Sports.
Mazishi ya marehemu huyo aliyeacha watoto kumi, yalihudhuriwa na mamia ya wananchi na wanamichezo mbalimbali, ambapo mwili wake ulisaliwa katika msikiti uliopo karibu na uwanja wa Amani, na baadae kupelekwa malazoni Chukwani. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu pahala pema Peponi. Amin.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.