Bajeti ya Wizara ya Afya
ambayo ilikuwa inajadiliwa katika
Mkutano wa bajeti unaondelea imerejeshwa tena katika Kamati ya Maendeleo ya
Wanawake na Ustawi wa Jamii , kwa ajili
ya marekebisho zaidi.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Pandu Ameir
Kificho amesema, Baraza la Wawakilishi limefikia uwamuzi huo baada ya
Wajumbe wengi kubaini mapungufu makubwa ya mgawanyo wa fedha katika
bajeti ya Wizara hiyo mwaka huu.
Spika Kificho ametowa ufafanuzi huo leo wakati akizungumza na
waandishi wa habari huko ofisini kwake Chukwani.
Amesema Wajumbe hao sio tu wamebaini kiasi kidogo cha fedha
zilizotengwa kwa ajili ya wizara hiyo mwaka huu, bali pia
maeneo ambayo sio kipaumbele cha Wizara yametengewa fedha nyingi
ukilinganisha na maeneo ya kutoa huduma
ambayo yametengewa kasma ndogo mno kiasi ambacho kitanguza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa
jamii kwa kiwango kikubwa.
Kwa hatua hiyo Mheshimiwa Spika ameagiza bajeti hiyo irudi
katika Kamati husika ili ikae tena na Wizara ya Afya pamoja na Watendaji wa
Wizara ya Fedha kwa lengo la kurekebisha mapungufu hayo kabla ya kuendelea kujadiliwa tena ndani ya
Baraza Jumanne ijayo.
Tukio hili linaonyesha jinsi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walivyo makini katika kuhakikisha bajeti ya Serikali inakuwa kwa maslahi ya
wananchi na si vinginevyo.
Hivi karibuni, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipatiwa
mafunzo kuhusu uchambuzi wa Bajeti
kupitia mradi wa Kuimarisha Vyombo vya Kutunga sheria (LSP) na umakini huo wa
Wajumbe katika kuijadili Bajeti ya Wizara ya afya unathibitisha namna mafunzo
hayo yalivyosaidia katika kuwajengea Wajumbe uwezo katika eneo hilo la kujadili na kupitisha bajeti.
No comments:
Post a Comment