Habari za Punde

Jahazi lazama, mmoja afariki

Na Khamisuu Abdallah
MTU mmoja amefariki dunia baada ya jahazi lenye namba za usajili 111 walilokuwa wakisafiria kuzama karibu na bahari ya kisiwa cha Chumbe.

Jahazi hilo lililokuwa likitokea Zanzibar kuelekea Tanzania Bara na kubeba mizigo pamoja na mabaharia watano, lilizama baada kutoka mbao na kujaa maji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna wa Polisi, Mkadam Khamis Mkadam, alimtaja marehemu kuwa ni Mohammed Khatib Mahadhi, ambae alikuwa ndie nahodha wa jahazi hilo.

Kamanda Mkadam alisema jahazi hilo lilikuwa limepakia vitu mbali mbali vikiwemo televisheni na baiskeli.
Alisema maiti ya nahodha huyo ilipatikana kando ya kisiwa cha Chumba usiku wa kuamkia jana ikielea.

Alisema tukio hilo lilitokea Mei 18 mwaka huu majira ya saa 4:00 za usiku katika maeneo ya kisiwa cha Chumbe.
Aliwataja walionusurika kuwa ni Juma Khatib Abdalla mkaazi wa Kiembesamaki, Habibu Haji Mussa, Twaha Amin Haji, Amin Abdalla Khamis na Seif Hassan Juma ambao hawakufamika mahala wanapoishi.

Aidha alisema manusura wapo salama na wanaendelea na shughuli zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.