Habari za Punde

Kilimo hatarini kuporomoka

Na Mwashamba Juma
SEKTA ya kilimo imetajwa kuwa hatarini kuangamia kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha maeneo mengi ya kilimo kuvamiwa na maji ya bahari,jambo ambalo linahatarisha usalama wa chakula.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kwa niaba ya rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema hayo wakati akizundua mkakati wa mabadiliko ya tabianchi katika hoteli ya Zanzibar Ocean View, Kilimani mjini, Unguja.

Alisena maeneo yaliyoko kwenye ukanda wa pwani, chini ya mita tano kutoka usawa wa bahari yako hatarini kuathirika kutokana na kuingia maji ya bahari kulikosababishwa na kupanda kwa kina cha bahari.

Alisema uchumi na maisha ya visiwa vya Zanzibar unaotegemea zaidi ustawi wa shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi, utalii na miundombinu, shughuli hizo ziko kwenye tishio la kuathiriwa na mabaidiko ya tabianchi. 

Alisema mabadiliko ya tabianchi yameathiri mfumo wa mvua kwa sekta ya kilimo, hali inayoathiri zaidi sekta hiyo pamoja na mazao kutokanana kukosekana mvua za kutosha au zenye viwango vikubwa ambazo zinaathiri ustawi wa mazao ya kilimo.


Aidha alisema jumla ya maeneo 148 yanayotegemewa kwa shughuli za kilimo yanaingia maji ya chumvi kutokana na kupanda kwa kina cha bahari ambapo Pemba 123 na Unguja 25 ambapo sasa fursa yakilimo zinapatikana kwa tabu.

Alisema mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya shughuli za wanaadamu za maisha yao ya kila siku katika kujitafutia riziki, ikiwemo ukataji misitu ovyo, umwagaji wa taka ngumu, uvuvi haramu na uchafu unaotokana na taka za wiwandani pamoja na uchafuzi wa hewa unaotokana na hewa mkaa.

Alisema kiasi cha hekta milioni 17  za ardhi kwa mwaka zinageuka kuwa jangwa duniani kote sambamba na kiwango cha joto kuzidi hadi nyuzi joto 4.5 ifikapo mwaka 2050 na kuongeza kuwa kina cha bahari kinatarajiwa kupanda hadi kufikia ujazo wa bahari 2.2 kutokana na kukithiri kwa joto kali.

Hivyo Zanzibar kama sehemu ya dunia alisema ina wajibu wa kuungana na nchi zote duniani kuadhimisha siku za mazingara kwa lengo la kutafakari kwa kina matatizo ya kimazingira yanayoikabili sambamba na kutumia fursa hiyo kuyatatua.

Alisema mkakati wa mabadiliko ya tabianchi uliozinduliwa unatoa tathmini juu ya athari za mabadiliko hayo pamoja na kubuni njia sahihi za kukabiliana na athari zake.

“Kimsingi mkakati huu unatoa tathmini ya mabadiliko ya tabianchi kwa Zanzibar pamoja na kutoa njia muhimu za kujihami na kukabiliana na athari hizo pamoja na kupunguza fursa za kukabiliana na ongezeko la hewa ukaa,” alisema.

Akizungumzia suala la utalii,alisema serikali ya Zanzibar imeamua kuufanya utalii kuwa sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar kutokana na kuwa na vivutio vingi ambavyo vina jumuisha mambo ya kale, historia, utamaduni na maliasili ambayo ni misitu ya hifadhi, fukwe na bahari.

Alisema vivutio hivyo vinaonekana kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, sambamba na hote nyingi zilizojengwa kabirbu na fukwe za bahari zinaonekana kuathiriwa na mmong’onyoko wa fukwe.

Uzinduzi wa mkakati wa mabadiliko ya tabianchi ulikwenda sambambana maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambapo ujumbe wa mwaka huu unasema ‘Sema usikike, ongezeko la kina cha bahari hakikubaliki.’

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.