Habari za Punde

Maalim Seif Azindua Jengo la JUDO Pemba

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk wakati wa uzinduzi huo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada, wakikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo la Judo, Gombani Chake Chake Pemba. 
Rais wa heshima wa mchezo wa judo Zanzibar Bw. Shima Oka, akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo hilo lililojengwa katika eneo la viwanja vya  Gombani Chakechake Pemba.
Baadhi ya vijana wakionesha umahiri wao wa mchezo wa karati wakati wa uzinduzi wa jengo la judo Gombani  Chake Chake Pemba. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Na Hassan.Hamad. OMKR 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameelezea kuridhishwa na umahiri unaooneshwa na vijana wa michezo ya judo na karate Kisiwani Pemba.

Amesema kutokana na umahiri walio nao, vijana hao wanaweza kushindana katika michezo ya kimataifa na kuweza kuibuka na ushindi mkubwa.

Mhe. Maalim Seif ameeleza hayo wakati akizindua jengo la judo, mkabala na uwanja wa Gombani Chake Chake Pemba.

Amesema Zanzibar imekuwa ikitajika sana katika mchezo wa judo kwa nchi za Afrika ya Mashariki na kati, na kwamba kukamilika kwa jengo hilo kutaamsha ari na mori kwa vijana wa Zanzibar na kuweza kuiletea sifa zaidi.

Amefahamisha kuwa kukua kwa michezo ya judo na karate kutachukua nafasi iliyokuwepo ya watu wengi kujishughulisha na michezo hasa watakapokuwa na uhakika wa ushindi wakati wachezaji wa Zanzibar watakaposhiriki katika mashindano ya kimataifa.

Amesema matarajio ya Serikali katika michezo hiyo ni kupatikana mabadiliko makubwa ya michezo itakayorejesha heshima ya Zanzibar katika kanda ya Kusini mwa jangwa la Sahara
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameongeza kuwa lengo kuu la serikali kuunda Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, ni kujaribu kuunganisha sekta zilizomo katika wizara hiyo kwa kufanya kazi pamoja na kuleta mafanikio zaidi.

Aidha amesema mbali ya kujenga afya na ukakamavu kwa vijana sekta ya michezo pia inaweza kuchangia maendeleo ya sekta ya utalii, kutoa ajira kwa vijana na hatimaye kusaidia kukuza uchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Mhe. Maalim Seif amesema iwapo vyama vya michezo vitafanya kampeni maalumu za kuwashawishi vijana kujiunga na michezo ya Judo na Karati, hamasa iliyopo sasa itaongezeka na kupelekea kuimarika kwa michezo hiyo.

Ameupongeza Ubalozi wa Japan nchini Tanzania pamoja na chama cha Judo Zanzibar kwa kufanikisha ujenzi huo pamoja na vifaa vya michezo ambavo ka pamoja vimegharimu shilingi milioni mia tano (500 milion).

Amewasisitiza wanamichezo kuungana ili kuleta maendeleo zaidi katika sekta ya michezo nchini.

Katika hatua nyengine Maalim Seif amewatanabahisha vijana kuwa makini na mashindano ya kombe la dunia yanayotarajiwa kuanza tarehe 12 mwezi huu nchini Brazil, kwa kutopoteza muda mwingi kushughulikia mashindano hayo, na kuacha shughuli zao kijamii ikiwa ni pamoja na kufanya ibada za usiku katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mapema akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk, amesema mradi wa jengo hilo ni miongoni mwa mikakati ya Wizara hiyo katika kukuza michezo nchini.

Amesema kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo, wanakusudia pia kuufanyia matengenezo uwanja wa michezo wa Gombani Pemba kwa kuweka TATAN ili uweze kutumika kwa michezo ya riadha.

Aidha amesema wanakusudia kujenga bwawa kubwa la kuongelea (swimming pool), ili liweze kuwasaidia vijana wanaotaka kushiriki mchezo huo na kuwawezesha kushiriki michezo ya Olimpiki duniani.

Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada, amesema iwapo vijana wa Pemba watafanikiwa kuingia katika michezo ya Olimpiki ya Kimataifa nchini Japan mwaka 2020, ofisi yake inaahidi kuwadhamini vijana hao.

Kwa upande wake, Rais wa heshima wa mchezo wa judo Zanzibar Bw. Shima Oka, ametoa wito kwa vijana wa Pemba kujiunga na mchezo wa Judo ili kuendeleza mafanikio yaliyokwisha patikana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.