Habari za Punde

Maalim Seif Afungua Mafunzo ya Majaji, Mahakimu,Wanasheria na Mawakili Zanzibar.

Na Hassan Hamad, (OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amevikumbusha vyombo vya sheria juu ya wajibu wa  kushirikiana na wananchi katika utekelezaji wa sheria, ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa watu wanaokabiliwa na kesi mahamani.

Mhe. Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika hoteli ya Zanzibar Ocean View, wakati akifungua mafunzo ya siku nne kwa majaji, mahakimu, wanasheria, mawakili pamoja na kada nyengine za sheria.

Amesema mara nyingi wananchi wamekuwa wakikosa haki zao mahakamani kwa madai ya kuwepo sababu mbali mbali zikiwemo uchelewaji wa kesi, kukosekana kwa mashahidi na mahakimu wa kundesha kesi hizo, na kutaka kuzingatiwa kwa mambo hayo ili kuondosha vikwazo vya kupatikana kwa haki miongoni mwa wananchi.

Amesema katika kufanikisha masuala hayo, ni lazima vyombo vinavyohusika kushirikiana kwa pamoja, ili kuona kuwa wananchi wanapata haki zao zinazostahiki kwa wakati muafaka.

Makamu wa Kwanza wa Rais, pia amesisitiza juu ya haki ya dhamana kwa washitakiwa wanaoweza kupewa dhamana kwa mujibu wa sheria, na kwamba kitu cha msingi ni kuwajengea mazingira bora washitakiwa hao ili waweze kufika mahakamani pale wanapohitajika.

Aidha amesisitiza haja ya kuzitazama sheria ambazo hazileti usawa na zenye ubaguzi ndani yake, ili ziweze kubadilishwa na wananchi washirikishwe katika mageuzi hayo.

Mapema akizungumza katika mafuzo hayo, Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mhe. Aboubakar Khamis Bakari amesema suala la uchelewashaji wa kesi halizihusu mahakama peke yake, bali kuna wadau wengi wakiwemo mashahidi na polisi ambao wanapaswa kushirikiana kikamilifu kuhakikisha kuwa tatizo hilo linaondoka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.