Na Husna
Mohammed
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdillah Jihad
Hassan, amesema serikali inakusudia kuimarisha shughuli za utafiti katika
masuala ya mifugo sambamba na kutoa elimu kwa wafugaji.
Alisema hayo
jana katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea mjini hapa wakati
akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2014/2015.
Alisema sekta
ya mifugo itaimarishwa ikiwa ni pamoja na kuvipatia dawa na vitetendea kazi
vituo vitatu vya utafiti.
“Tutafanya
utafiti wa kuangalia uzalishaji wa kuku chotara wa nyama na kabila ya kiasili
ya kuchi, kufanya utafiti juu ya vikwazo vya ufugaji mbuzi katika kijiji cha
Kiuyu Mbuyuni,” alisema.
Aidha alisema
wataimarisha utoaji wa elimu kwa wafugaji katika nyanja za utunzaji, uzalishaji,
usarifu wa bidhaa za mifugo na masoko kwa kuwawezesha wasaidizi mabwana mifugo
20 kuwafikia wafugaji wapatao 20,000.
Alisema
katika mwaka huo wa fedha wanatarajia kuongeza uzalishaji wa mifugo na matumizi
bora ya mazao ya mifugo kwa kuanzisha mashamba yapatayo 40 ya malisho katika
eneo la Kizimbani.
“Tutalima na
kupanda jumla ya eka tano za majani katika kituo cha malisho huko Kizimbani na
shamba la Chamanangwe kisiwani Pemba pamoja na kuchangia gharama za ujenzi wa
mitambo 10 ya biogesi,” alisema.
Wizara hiyo
imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 11,591,053,000 kwa ajili ya matumizi ya
wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Kwa upande
wake, Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari,imesikitishwa na wizara
hiyo kwa kutoweza kutayarisha sera ya uvuvi na mazao ya baharini.
Mjumbe wa
kamati hiyo, Mhe. Amina Iddi Mabrouk, akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, katika
kikao cha baraza la wawakilishi, alisema kamati imesikitishwa na kutotayarishwa
kwa sera hiyo jambo ambalo linaonesha serikali ni nzuri ya kupanga lakini
inakosa umakini wa kutosha wa utekelezaji wa mipango yake.
“Kazi hii
haikufanyika kwa madai ya kukosa nyenzo ambapo kamati imeelezwa kwamba kazi hii
inatarajiwa kutekelezwa katika mradi wa SMART Fish,” alisema.
Sambamba na
hilo kamati hiyo pia imesema imesikitishwa kwa kutoongezeka makusanyo ya leseni
za uvuvi wa ndani na nje na kufikia
kiwango sawa cha makusanyo kama ya mwaka jana.
Aidha kamati
hiyo iliitaka wizara kuongeza nafasi za uzalishaji wa ajira 120 kwa vijana
kupitia mradi wa kuendeleza wafugaji wadogo.
Kamati hiyo
pia ilitoa wito wa kutekeleza sekta ya mazao na mifugo kwa kuimarisha utoaji wa
huduma za mifugo kwa jamii pamoja na kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa
kutumia mikakati mbalimbali.
Akichangia
hotuba ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwakilishi Asaa Othman (Wete), alisema sekta ya uvuvi inakabiliwa na changamoto kubwa
juu ya wafugaji na wajasiriamali kukosa mitaji ambayo itawawezesha kufikia
malengo waliojiwekea.
Alisema wafugaji
ni lazima wabadilike kwa kupatiwa taaluma bora ya ufugaji kwani kufanya hivyo
kutapelekea kupunguza maradhi.
Akizungumzia
suala la utumishi, alisema ni vyema wafanyakazi kupatiwa mafunzo endelevu ya
kikazi ili kwenda na wakati wa sayansi na teknolojia.
Nae
Mwakilishi wa jimbo la Kojani, Mhe. Hassan Hamad, alisema sheria ya uvuvi ya
nambari 7 ya mwaka 2010 kwa mahitaji ya sasa imepitwa na wakati na inahitaji
marekebisho makubwa.
Mwakilishi wa
nafasi za wanawake, Kazija Kona, alisema wakati umefika sasa kwa serikali
kuwaendeleza vijana wa kizanzibari katika sekta ya uvuvi.
No comments:
Post a Comment