Habari za Punde

Balozi Seif awatembelea Wazee wasiojiweza waliopo katika nyumba za Serikali Welezo na Sebleni

 Baadhi ya Wazee wa nyumba za Serikali za Welezo wakifutilia maelezo ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seifhayupo pichani wakati  alipowatembelea kwenye makazi yao.
 Balozi Seif akigawa zawadi kwa mmoja wa wazee wa Welezo alipowatembelea na kuwafariji wakiwa ndani ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

 Baadhi ya Wazee wa nyumba za Sebleni wakifuatilia hotuba ya Balozi Seif hayupo pichani wakati akijiandaa kuwapatia zawadi kwa ajili ya siku kuu ya Iddi el Fitri.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na baadhi ya wazee wa kike wanaotunzwa katika nyumba za Serikali zilizopo Sebleni Mjini Zanzibar.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akitoa zawadi kwa Wazee wa kiume wa Sebleni
Balozi Seif akiagana na wazee wa Sebleni mara baada ya kuwasalimia na kuwapatia zawadi kwa ajili ya kusherehekea vyema siku kuu ya Iddi el Fitri.

Mzee Omar Said wa Nyumba za Sebleni kwa niaba ya wazee wenzake wa Sebleni na Welezo akimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar hayupo pichani kwa juhudi zake za kufuatilia changamoto zinazowakabili wazee hao.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ
 
Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwa na wajibu na jukumu kubwa la  kuwatunza na kuwathamini wazee wasiojiweza hivi sasa kutokana na mchango wao mkubwa walioutoa kwa  nchi hii wakati wa kulitumikia Taifa lao.
Alisema mchango wa wazee hao umekuwa ukiendelea kutumiwa na wananchi walio wengi hapa nchini ikiwemo kigezo cha amani na utulivu  kinachotokana na juhudi za wazee hao wakati wa kupigania utu wa mwafrika.
 
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa ziara yake fupi ya kuwasalimia Wazee wanaotunzwa katika Nyumba za Serikali za Welezo na Sebleni na kuwapatia zawadi ya nguo kwa ajili ya kusherehekea vyema siku Kuu ya Iddi El Fitri inayotarajiwa kufanyika mapema wiki ijayo.
 
Alisema wazee wa Taifa hili wametumia muda wao mkubwa wa kujenga mazingira bora ili kizazi chao kiendelee kuishi kwa amani na furaha tofauti na enzi zao zilizokumbwa na mitihani ya kutawaliwa jambo ambalo liliwakosesha uhuru wa kidemokrasia wa kufanya wanalolihitaji katika maisha yao.


“ Sisi kama Viongozi wa Serikali bado tunathamini na kuheshimuj wazee wetu waliotumia muda wao mkubwa wa kulitumikia Taifa letu kazi ambayo kwa sasa tunafaidika nayo “. Alisema Balozi Seif.
 
Akigusia suala la mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaahidi Wazee hao wa Welezo na Sebleni kwamba ule utaratibu wake wa kufutari nao pamoja utaendelea kama kawaida penye majaliwa kwa miaka ijayo.
 
Balozi Seif aliwafahamisha wazee hao kwamba mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani wa mwaka huu ilishindikana kufutari nao pamoja kutokana na kutingwa na majukumu mengi  ya kitaifa.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapatia zawadi ya madira na mitandio yao wazee wa kike na wale wazee wa kiume wakafaidika na kivazi cha asili cha kiko na fulana zake ili wazitumkie siku ya furaha ya iddi el fitri.
 
Akitoa skurani kwa niaba ya wazee hao wa Welezo na Sebleni Mzee Omar Said alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa juhudi zake za kuendelea kufuatilia changamoto zinazowakabili wazee hao.
 
Mzee Omar alisema juhudi hizo zimekuwa zikiwapa faraja wazee hao na kuendelea kujenga imani kwa Serikali ambayo inaelewa mchango wao katika ukombozi wa Visiwa hivi.
 
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji,Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto Bibi Asha Abdulla alisema Nyumba za Wazee ziliopo Welezo zimekuwa zikihudumia wazee wapatao 42 ambao kati yao wanawake wapo 14 wakati wazee wa Kiume wanafikia 31.
 
Kwa upande wa Sebleni Katibu Mkuu Asha alisema Nyumba hizo zinahudumia wazee 46 ambao kati ya hao wazee wa kike wanafikia 29 na wale wa Kiume wapo idadi ya 17 wakiwa chini ya usimamizi wa Idara ya Ustawi wa Jamii iliyopewa jukumu la kuwahudumia wazee hao.
 
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.