Habari za Punde

Dk Shein aagiza Bonde la Cheju libaki kuwa la kilimo tu


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                    24 Julai, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezitaka wizara zinazohusika na Kilimo, Ardhi, miundombinu na mazingira kuhakikisha kuwa bonde la Cheju haligeuzwi kuwa eneo la makaazi ya watu.

Akizungumza huko katika kijiji cha Cheju Mkoa wa Kusini Unguja leo mara baada ya kuzindua skuli ya maandalizi ya kijiji hicho, Dk. Shein ametahadharisha juu ya tabia ya wananchi kuyageuza maeneo ya kilimo kuwa ya makazi.

Alieleza kuwa ujenzi wa barabara ya Jendele hadi Unguja Ukuu Kaibona kupitia bonde la Cheju inayojengwa kwa kiwango cha lami unaweza kuvutia wananchi kuanzisha makaazi katika bonde hilo hivyo tahadhari hazina budi kuchukuliwa kulinda bonde hilo.

Dk. Shein amezitaja Wizara hizo kuwa ni Kilimo na Maliasili, Miundombinu na Mawasiliano, Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Kwa hivyo ameziagiza Wizara hizo kuhakikisha kuwa bonde la Cheju linabaki kuwa eneo la kilimo na kuwa utaratibu wa kulipima na kuliwekea mipaka bonde hilo hauna budi kufanyika.

Dk. Shein alibainisha kuwa bonde la cheju lenye ukubwa upatao hekta 2,100 limo katika mpango wa Serikali wa kuimarisha kilimo cha mpunga cha umwagiliaji ili kutekeleza lengo la Serikali la kujitosheleza kwa chakula hasa mchele.

Alifafanua kuwa mradi wa uendelezaji wa bonde hilo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji umo mbioni kuanza kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Korea hatua inatarajiwa kuongeza tija katika kilimo cha mpunga.

Dk. Shein alieleza kuwa Lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa chakula hususan mchele hadi kufikia asilimia 50 ya tani 80,000 zinazoagizwa hivi sasa kutoka nje kila mwaka ifikapo msimu wa mwaka 2016/2017.

Aliwaambia wananchi hao kuwa lengo hilo linakaribia kufikiwa kutokana na jitihada za wakulima pamoja na utaratibu wa serikali wa kutoa ruzuku kwa wakulima kwa asilimia 80 kwenye huduma za kilimo ikiwemo mbolea, mbegu, matrekta na madawa ya kuulia wadudu na magugu.

Alitoa mfano wa mafanikio hayo ni ongezeko la uzalishaji wa mpunga kutoka tani 6,000 mwaka 2012 hadi tani 33,000 mwaka 2013.

Kuhusu utekelezaji wa ahadi mbalimbali kwa wananchi wa Cheju, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema ahadi hizo zimeanza kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Jendele kupitia Cheju hadi Unguja Ukuu kwa kiwango cha lami.

Suala la maji aliwaeleza wananchi hao kuwa ahadi hiyo imeanza kutekelezwa chini ya mpango wa kuipatia maji wilaya ya Kati ambapo hivi sasa ujenzi wa miundombinu unaendelea kufanyika.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.