Na Kauthar Abdalla
JUMUIYA ya Kuhifadhi Mazingira Ras Fumba
(FUPECO),imeeleza kusikitishwa na tatizo la uharibifu wa mazingira unaofanywa
katika eneo hilo .
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti
wa Jumuiya hiyo, Maria Shoka Hassan ,alisema
tatizo la uharibifu wa misitu katika maeneo ya ghuba ya Minai limekuwa kubwa na
kupoteza rasilimali ya msitu.
Alisema katika visiwa vya Kwale,Nyemembe
na maeneo ya karibu hali imekuwa mbaya kutokana na kuvamiwa na kukatwa miti ya
asili.
Alisema waharibifu wakubwa ni watu wa
vijiji vinavyozunguka ghuba hiyo pamoja na watu kutoka maeneo mengine.
Alisema licha ya jitihada za kuwaelimisha
wananchi juu ya umuhimu wa kuwepo misitu na uhifadhi wake , bado kuna ongezeko
la uharibifu wa misitu ya asili.
Aliiomba serikali kupitia Idara ya misitu
na mali asili
zisizorejesheka kuandaa mikakati imara ya kuwadhibiti wahalifu ili kunusuru mali asili.
Kwa upande wake, Msaidizi Ofisa Misitu
Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka, Yussuf Haji Kombo, alisema kutokana
na sheria eneo la msitu lolote linashughulikiwa na kijiji husika na
inaposhindikana Idara inaweza kuchukua hatua.
No comments:
Post a Comment