Na Masanja Mabula,Pemba
WAKULIMA wa karafuu waliokopeshwa fedha
na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC)
katika wilaya ya Wete huenda wasipate mikopo ya fedha kwa msimu huu
iwapo watashindwa kurejesha mikopo hiyo waliyokopeshwa msimu uliopita.
Akizungumza na masheha wa wilaya
hiyo ofisini kwake, Mkuu wa wilaya ya
Wete, Omar Khamis Othman, alisema shirika la ZSTC linadai shilingi milioni 23
kutoka kwa wakulima wa karafuu wa wilaya hiyo fedha ambazo walikopeshwa msimu
uliopita.
Alisema katika msimu uliopita shirika
lilikopesha wakulima wa karafuu katika wilaya hiyo zaidi ya shilingi milioni
138 ambapo fedha ambazo hadi sasa zimerejeshwa ni shilingi milioni 115.12.
Aliwataka Masheha kuzifuatlia fedha hizo
kwa wakulima waliokopeshwa na kuwahimiza kurejesha fedha hizo ili kuliwezesha
shirikia kuendesha shughuli zake za kuwahudumia wakulima kwa ufanisi zaidi.
Aidha alisema serikali ya wilaya hiyo
inakusudia kuwaita wadaiwa ambao wameshindwa kurejesha mikopo ambapo hiyo
itakuwa ni hatua ya kwanza na iwapo wataendelea kukaidi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine aliwataka masheha
kuwa waadilifu katika kusimimia suala la ujazaji wa fomu kwa wananchi watakao
hitaji kukopeshwa na shirikia katika msimu huu wa mavuno.
Nao baadhi ya masheha waliahidi kusimamia
uadilifu ili kuona zoezi la ukopaji wa fedha linafanikiwa na wanaokopeshwa ni
wale ambao wana uwezo wa kurejesha kwa wakati.
No comments:
Post a Comment