HOTUBA
YA MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA MHE. SAMUEL SITTA KATIKA UFUNGUZI WA
AWAMU YA PILI YA BUNGE HILO, DODOMA TAREHE 5 AGOSTI 2014
Karibuni tena Dodoma Waheshimiwa Wajumbe wa
Bunge Maalum la kutunga Katiba ya nchi yetu. Sote tuna kila sababu ya kumshukuru
Mwenyezi Mungu wetu kwa kuendelea kutupa uhai na afya hadi leo kutuwezesha kuwepo
ndani ya ukumbi huu. Tupo humu ili tuitekeleze kazi waliyotukabidhi Watanzania
wenzetu milioni arobaini na sita (46) ya kuwapatia Katiba mpya. Dhamana hii ni
nzito na haistahili kufanyiwa ajizi.
Tunaendelea na shughuli zetu za Bunge Maalum
kwa kuzingatia Kanuni ya 30 (1) inayosema
"Akidi
kwa kila kikao cha Bunge Maalum isipokuwa wakati wa kupitisha uamuzi wa Bunge
Maalum itakuwa ni nusu ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum".
Nimetaarifiwa na Katibu kwamba wajumbe waliokuja
Dodoma kuhudhuria ni zaidi ya robo tatu ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum. Nawashukuruni
nyote kwa kuja hapa Dodoma ili kutimiza wajibu wenu.
Kwa niaba yenu, nawashukuru Watanzania wenzetu
wote ambao kwa mamilioni wamedhihirisha utashi mwema wa kisiasa kwa kuunga
mkono hatua ya Bunge Maalum kuendelea na kazi zake hadi tuipate Katiba
inayopendekezwa ambayo wataipigia kura ya maoni. Kipekee na kwa niaba yenu,
nawashukuru kwa dhati viongozi wetu wa dini wa madhehebu yote wanaloliombea
Taifa hili mafanikio Bunge Maalum, wakitanguliza utaifa pamoja na amani ya nchi
na umoja ndani ya nchi na siyo ubinafsi na maslahi ya makundi.
Kwa leo sikupenda sana kuzungumzia hoja mbali
mbali zinazotawala magumzo ya mchakato wa Katiba mpya hapa nchini, magumzo
yanayoendeshwa na makundi maalum kwa jazba na hata matusi. Hata hivyo
nalazimika kutoa maelezo ya ufafanuzi kuhusu upotoshaji mkubwa unaoendeshwa na
baadhi ya watu kuhusu Bunge Maalum. Nikiwa Mwenyekiti wenu ninao wajibu wa kuwafafanulia
wananchi kuhusu uhalali wa shughuli za Bunge Maalum linaloendelea na utaratibu
wa shughuli zetu.
Ni
Rasimu ya Tume au la
Wapo wanaodai kuwa eti hapa Bungeni hatujadili
Rasimu ya Tume. Tuhuma hii haina ukweli hata kidogo. Msingi wa majadiliano yote
tangu tumeanza ni Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Katiba. Utaratibu
ni kwamba pale ambapo wajumbe wanaona panafaa kurekebishwa wanafanya hivyo.
Maana ya rasimu ni andiko ambalo halijajitosheleza bila kupata ithibati ya
taasisi ya juu zaidi. Anayekabidhiwa rasimu anayo haki na mamlaka ya
kuirekebisha. Vinginevyo kujadili rasimu hakuna sababu. Itakuwa ni jambo la
ajabu na lisilo na mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka ya kujadili
Rasimu ikishaijadili iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati ilipowasilishwa!
Je
suala ni muundo wa Muungano tu?
Maudhui ya Rasimu yanajumuisha baadhi ya
masuala muhimu yafuatayo:
- Kuimarisha
Muungano wetu kwa kuleta uwiano bora
zaidi wa mamlaka ya Zanzibar na Tanzania Bara
ndani ya Muungano
- Kuimarisha
haki za binadamu ili kuwawezesha raia
wa kawaida kufaidi uhuru wa demokrasia bila
ubabe na dhuluma
- Kuzuia
wachache kufuja rasilimali za taifa bila kujali
maslahi ya wengi na ya vizazi vijavyo.
- Kujenga
uwiano sahihi na wenye haki baina ya wanawake
na wanaume katika nafasi za uongozi.
- Kubainisha
hatua zenye kuleta matumaini mapya ya
maendeleo kwa makundi maalum ya vijana wakulima
wadogo, wafugaji, wafanyakazi wa ngazi za
kawaida, walemavu, wafanya biashara wadogo na
wajasiriamali wengine.
- Kuweka
msingi imara wa kutungwa kwa sheria kakamavu
za kuzuia ukandamizaji wa raia, unyonyaji,
wizi wa mali ya umma, rushwa, hujuma
dhidi ya uchumi na kuzuia mapato haramu
na fedha chafu.
- Kutambua
haki za ardhi kwa wakulima, wafugaji na
wajasiriamali wengine ili kupunguza migongano
na migogoro.
- Kuweka
Misingi ya utawala bora inayozingatia uadilifu,
sifa stahiki na ufanisi.
- Kuwezesha
kutungwa kwa sheria bora zaidi zitakazosimamia
chaguzi zilizo za haki na huru zaidi
pamoja na kuwepo Tume za Uchaguzi zilizoboreshwa.
Zaidi ya hivyo, yapo mapungufu katika Rasimu
iliyopo kwa kuachwa masuala ya kuwezesha Serikali za mitaa; kutoa maelekezo
kuhusu masuala ya matumizi ya ardhi na rasilimali nyingine za Taifa. Nini
kinatuzuia kuiboresha Rasimu kwa kuyaongeza mambo haya ndani ya Katiba kwa
faida ya Taifa?
Yote haya ni masuala muhimu ambayo yamo ndani
ya rasimu na wakati wake wa kuyaweka sawa ndiyo huu. Pamoja na umuhimu wake
suala la muundo wa Muungano si suala la kutulazimisha tuyaahirishe mazuri yote
yaliyomo katika Rasimu tuliyopewa.
Uhalali
wa Shughuli za Bunge Maalum
Pamoja na uhalali wa kisheria wa Bunge hili
Maalum kuendelea kufanya kazi zake, linao pia uhalali wa kisiasa kutokana na
sifa za uwakilishi wetu na pia maudhui yaliyomo ndani ya Rasimu. Kutofautiana
maoni hakuwapi hadhi tofauti baadhi ya wajumbe kujiona wao wana uhalali zaidi
mbele ya wananchi kuliko wenzao. Ndiyo maana utaratibu umewekwa wa kupiga kura
na wa maridhiano. Utamaduni mpya unaoanza kujengwa na baadhi ya viongozi wa jamii
wa kususia mijadala halali na kwenda nje kuelezea hoja za upande mmoja hauna
nafasi katika Tanzania jamii isiyotaka fujo na utengano.
Wajumbe wa Bunge Maalum wanaoendelea na kazi
mjini Dodoma ni wateule wa Rais kwa niaba ya wananchi kwa kazi ya kutunga
Katiba. Kazi hii haiwezi kusitishwa kwa sababu tu wajumbe wachache wameisusia.
Tutazingatia matakwa ya sheria katika kufikia hatma ya mchakato wa Katiba.
Mabadiliko
ya Kanuni
Kama nilivyoeleza hapo mwanzo, Rasimu ina
jumla ya sura kumi na saba (17) zenye mambo mengi yenye maslahi kwa Watanzania
wote. Kwa muda tuliopewa wa siku sitini (60) isingewezekana kuikamilisha kazi
tuliyopewa ndani ya muda. Ikumbukwe kwamba kwa Kanuni zilivyo, kila sura mbili
zinahitaji siku tisa kuzifanyia kazi. Kwa njia hiyo, ingetuchukua siku takriban
mia moja thelathini (130) ili kuikamilisha kazi hii! Pendekezo la msingi hapa
ni kwamba Kamati zetu kumi na mbili (12) zizingatie na kuzijadili sura kumi na
tano (15) za Rasimu na pia zikamilishe uandishi wa sura mbili zilizojadiliwa awali
na ikibidi ziongeze sura ambazo zitadhihirika kuwa ni muhimu. Naamini mtiririko
huu utatuwezesha kuwa na mpangilio bora zaidi wa sura na ibara katika Katiba
mpya. Tusingependa na wala isingefaa kuomba tena muda wa ziada wa kazi ya
Katiba ndio maana tunafanya mabadiliko ya Kanuni. Kamati ya Uongozi iliyoketi
Dar es Salaam tarehe 28 Julai 2014 imependekeza yafanywe mabadiliko ya Kanuni
za Bunge Maalum kuwezesha kazi ikamilike ndani ya muda tuliopewa. Kwa hiyo
nitawaomba tuyatafakari mapendekezo ya mabadiliko ya Kanuni na hatimaye
kuyapitisha ili ratiba ya kazi zetu iende sawa. Nitawaomba muikubali ratiba
iliyogawanywa leo na pia mkubali kuzibadilisha Kanuni kwa lengo nililolieleza
hapa.
HITIMISHO
Pamoja na maoni ya kila namna yanayoendelezwa
kujadili mchakato wa Katiba nje ya Bunge hili, ni muhimu wahusika wapunguze
jazba, chuki na upotoshaji. Bunge Maalum lisaidiwe kwa mawazo chanya ili
limalize kazi yake.
Sisi tuliomo humu katika Bunge Maalum tuna
wajibu wa kuifanya kazi yetu kwa umakini na kwa uadilifu ili kazi yetu iwe
bora. Tujadiliane kwa uungwana. Tofauti za mawazo zisitufanye tuingize chuki na
maneno yasiyofaa. Katika mabadiliko ya Kanuni nashukuru sasa Kiti kimepewa
mamlaka ya kushughulikia utovu wa nidhamu ndani ya wakati. Lakini ninaamini
haitakuwa lazima kwangu mimi au Makamu Mwenyekiti kutumia nguvu za mamlaka yetu
ila tu pale itakapobidi.
Nawatakia nyote Mkutano wenye mafanikio kwa
maslahi mapana ya nchi yetu.
MUNGU
IBARIKI TANZANIA!
Samuel Sitta - MB
MWENYEKITI
BUNGE MAALUM LA KATIBA
No comments:
Post a Comment