Habari za Punde

Maalim Seif akutana na Balozi wa Uholanzi Ofisini Kwake leo

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Jaap Frediriks, alipofika Ofisini kwake migombani Zanzibar leo 21-8-2014.(Picha na Salmin Said).



 
 
 
 
 
 
 
 
Na Khamis Haji OMKR.
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema jambo muhimu litakalo zingatiwa na Zanzibar wakati itakapoanza shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ni kuona zinanufaisha wananchi na haziwi chanzo cha uharibifu wa mazingira.
 
Maalim Seif amesema hayo leo huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Jaap Frederiks.
Amesema anaamini kikwazo cha Kikatiba ambacho kinazuia shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa upande wa Zanzibar kitapatiwa ufumbuzi sio muda mrefu ujao, na baadaye Zanzibar itaanza kukaribisha wawekezaji mbali mbali kufanya shughuli hizo.


Amemweleza Balozi huyo kuwa tayari Zanzibar imeshaamua mafuta na gesi asilia liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano, hivyo kinachosubiriwa hivi sasa ni kukamilishwa taraibu za kisheria ambazo anaamini zinaweza kukamilishwa katika muda sio mrefu.

Hata hivyo, Maalim Seif amesema suala la uwezo na uzoefu litapewa umuhimu wa kipekee kwa kampuni zitakazo karibishwa kuwekeza katika sekta hiyo, ili kuhakikisha inakuwa sekta yenye mafanikio makubwa itakayoweza kuwasaidia ipasavyo wananchi wa Zanzibar katika  kuondokana na hali za umasikini, na sio kusababisha majanga ya kimazingira.

Maalim Seif amemweleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga vizuri kuhakikisha neema hiyo ya mafuta na gesi asilia haiwi chanzo cha uharibifu wa mazingira na uharibifu wa asili ya Zanzibar, ambayo ina mandhari ya kuvutia katika maeneo ya baharini na nchi kavu.


Akizungumzia maendeleo ya mchakato wa utafutaji Katiba Mpya, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema kutokana na hali iliyojitokeza hivi sasa suala la maridhiano baina ya pande zinazotafautiana ndilo pekee litakalowezesha kupatikana Katiba iliyo bora.


“Mimi binafsi ni muumini wa Maridhiano, kwenye Maridhiano kati ya pande zinazo zozana hakuna kitu kisichowezekana”, alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.


Maalim Seif katika mazungumzo hayo aliwakaribisha wawekezaji vitegauchumi kutoka Uholanzi kuja kufungua miradi yao Zanzibar katika sekta mbali mbali, ikiwemo kilimo cha maua, Utalii na ufugaji, ambapo nchi hiyo ina uzoefu mkubwa katika nyanja hiyo.


Amesema sekta hizo mbali na kuwanufaisha wawekezaji pamoja na nchi mbili hizo, lakini pia zitaweza kutoa fursa nyingi za ajira kwa wananchi, hasa vijana na kuwawezesha kumudu maisha yao.


Naye, Balozi wa Uholanzi nchini, Jaap Frediriks amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika nyanja tafauti, na kuendeleza miradi iliyokwisha anzishwa, ikiwemo matengenezo ya hospitali, utafiti wa bandari mpya, Uhifadhi wa mazingira na Uhifadhi wa Asili ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.


Balozi Frediriks ameihimiza Zanzibar kuwa na uwakilishi katika mkutano mkubwa wa Uwekezaji unaotarajiwa kufanyika nchini Uholanzi hivi karibuni, ili kuweza kujitangaza yenyewe kiuwekezaji hasa Utalii, sekta ambayo ina nafasi kubwa ya kuinua uchumi na maendeleo ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.