Habari za Punde

Magavana PTA kukutana Dar.

Na Eleuteri Mangi, Maelezo

Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini mwa Afrika (PTA) itakutana jijini Dar es Salaam.

Hayo yalibainishwa jana mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mkutano huo utakaofanyika mwishoni wiki hii.

“Huu ni mkutano wa kawaida wa mwaka wa Bodi ya Magavana wa nchi wanachama pamoja na Mawaziri wa Fedha, Tanzania ni mwanachama ndio maana mkutano wa 30 unafanyika hapa,” alisema.

Alisema katika mkutano huo mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo masuala ya fedha na uchumi, maendeleo ya benki ya PTA na mafanikio yake kwa nchi washirika.

Alisema sio kweli kwamba Tanzania haikopesheki bali deni lililopo linahimilika.

Aidha alisema PTA ni benki ya kiafrika na inafanyakazi nzuri ambapo inaonesha inakua kwa zaidi ya asilimia 30 kwa mwaka kwa miaka kadhaa hadi sasa na imekuwa na mizania ya dola za Kimarekani mil. 2.8 ikiwa miongoni mwa benki za maendeleo zinazofanya vizuri katika bara hilo.

Alisema mkutano huo utatanguliwa na semina ya wafanyabiashara itakayofanyika Agosti 21 siku moja kabla ya mkutano mkuu ambapo serikali itawakilishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

Kwa upande wake Rais na Mtendaji Mkuu wa benki  hiyo, Admassu Tadesse, alisema  Tanzania imekuwa mstari wa mbele na ni mwanachama hai ambapo imekuwa mfano mzuri kwa nchi wanachama kwa kutoa michango mbali mbali kwa wakati.


Benki ya PTA ilianzishwa mwaka 1985 ambapo hadi sasa ina jumla ya wanachama 22 ikiwemo nchi 18 ambazo ni Burundi, Comoros, Djibouti Congo, Kenya na Malawi.

Nchi nyinine ni Misri, Eritrea, Ethiopia, Mauritania, Rwanda, Seychelles, Somalia, Sudan, Uganda, Zambia, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania.

Aidha, PTA inashirikiana na nchi nyingine nje ya bara la Afrika ambazo ni Belarus na China.

Washirika wengine ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kampuni ya Bima ya Mauritia iitwayo Eagle na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Mauritius.


Mkutano wa mwaka huu unafanyikia Tanzania ikiwa ni utaratibu wa benkiya PTA kufanya mikutano ya mwaka kwa mzunguko ambapo washiriki watakuwa Mawaziri wa Fedha, Magavana wa nchi wanachama, sekta binafsi, Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali nchini na Wawakilishi wa Mashirika ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.