Na Fatina
Mathias, Dodoma
Kamati Kuu ya
Chama Cha Mapinduzi(CC) iliyokutana mjini Dodoma, chini ya Mwenyekiti wake Rais
Jakaya Kikwete, imeridhishwa na mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba na mijadala
na hivyo kulibariki kuendelea na kazi yake.
Mbali na hilo pia imeagiza
wanachama wake Mawaziri na Wabunge wasiohudhuria vikao vya bunge maalumu
wahudhurie mara moja.
Kamati hiyo
pia, imetangaza kuanzia sasa ziara za Rais zitakuwa na mawaziri wachache ili
kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika vikao vya bunge hilo vinavyoendelea,
ili kufanikisha upatikanaji wa katiba yenye maridhiano.
Akisoma
maazimio ya CC kwa waandishi wa habari,Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye, alisema wanachokihitaji ni kuhakikisha wanamaliza jambo hilo lililopo
mbele yao na kuendelea na mambo mengine, sio rahisi wajumbe kuhudhuria wote
katika vikao hivyo.
Alisema Kamati
Kuu imeeleza kuridhishwa na maendeleo ya majadiliano na upigaji kura katika
Bunge hilo .
“CC inawahimiza wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba, kuhudhuria vikao vya kamati na vile vya Bunge na kushiriki katika
mijadala kwa kutanguliza masilahi mapana ya taifa na hatimaye kuipatia nchi katiba
inayotarajiwa na Watanzania wote,” alisema.
Alisema CCM
inaridhishwa na namna wajumbe wa bunge maalumu wanavyoshiriki mijadala na
kujenga hoja, pia wanavyoshughulikia mitazamo tofauti katika majadiliano yao na upigaji kura.
Hata hivyo,
alisema Kamati Kuu imemuagiza Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuendelea kukutana na vyama vya siasa vilivyokuwa
katika mazungumzo ya maridhiano yaliyovunjika chini usimamizi wa Msajili wa vyama
vya siasa nchini.
“Hata hivyo Kamati Kuu imesikitishwa na
kuvunjika kwa mazungumzo kati ya CCM, CUF, CHADEMA na NCCR-Mageuzi,”alisema Nnauye.
Kuhusu juhudi
zinazofanywa na Kituo cha Demokrasia nchini(TCD), Kamati Kuu ilipongeza
ushiriki wa Katibu Mkuu Kinana na vyama wanachama wa TCD, katika juhudi
zinazolenga kuimarisha amani, utulivu, mshikamano na kuaminiana.
Alisema Kamati
Kuu inaendelea kuwasii Watanzania wote kuendelea kushikamana na kuvumiliana,
pale wanapopishana kimtazamo juu ya hoja mbali mbali za katiba.
“Tuvumiliane
kwani amani, utulivu na utanzania wetu ni muhimu kuliko tofauti zetu za
kimtazamo,” alisema.
No comments:
Post a Comment