Habari za Punde

WanaCUF watakiwa kuhamasishana kupata vitambulisho vya ukaazi ZAN ID


Na Khamis Haji, OMKR

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kuanzisha mitandao ya kupeana taarifa kuhamasishana na kusaidiana kutafuta vitambulisho vya kupigia kura kwa wasiokuwa navyo, kama hatua ya maandalizi ya ushindi mkubwa wa chama hicho mwaka 2015.

Maalim Seif amesema iwapo wanachama watahakikisha kila moja ameandikishwa kuwa mpiga kura, ushindi wa CUF utakuwa wa kishindo na hakuna atakayeweza kuwaibia kura au kuchezea matokeo ya uchaguzi hapo mwakani.

Amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa Baraza ya CUF ya Msumbiji iliyopo Magogoni, Wilaya ya Mgharibi Unguja.

Katibu Mkuu amesema chama cha CUF kimezidi kukubalika miongoni mwa wananchi walio wengi Zanzibar na kinachohitajika ni kuhakikisha wanachama na wote wanaokiunga mkono wanamiliki vitambulisho vya kupigia kura vitakavyo wawezesha kupiga kura mwakani.


“Kama CUF ni shamba basi miti yake kila siku inazidi kunawiri, sina wasi wasi ushindi upo, kama 2010 tulishindwa kwa kura 3000 kwa hesabu za Tume, tujipange vizuri tupate ushindi mkubwa ambao hauwezi kuchezewa au kubadilishwa”, alihimiza.

Amesema utaratibu wa kuanzisha Mabaraza ya wanachama unatoa mchango mkubwa katika kukiimarisha chama hichp na umekuwa ukikisaidia sana chama kueneza taarifa zake kwa wanachama kwa urahisi na kwa haraka, hivyo chama kitahakikisha unaendelezwa.

Aidha, amesema Mabaraza hayo ni njia moja wapo ya kuwawezesha wanachama kujuana na kusaidiana, ikiwemo katika suala la kupata vitambulisho vya ukaazi Zanzibar (ZAN ID), ambapo hadi sasa kuna idadi kubwa ya wanachama wakiwemo vijana ambao hawana vitambulisho hivyo.

Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amewataka wanachama na wananchi wote wa Zanzibar wasidharau kutafuta vitambulisho vya ZAN ID kutokana na umuhimu wake katika maisha ya kila siku, licha ya kuwawezesha kupata haki zao za kupiga kura.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema chama kitapita kila Wilaya kuhamasisha wanachama wasiokuwa na ZAN ID kuvitafuta, ili viweze kuwasaidia katika shughuli zao za kijamii na kimaendeleo, pamoja na kuwawezesha kupata fursa za kuchagua viongozi.

Amesema baadhi ya wakati wanachama hukosa vitambulisho hivyo kutokana na usiri wa kuvifuatilia katika sehemu husika, hivyo chama hicho kimeamua kuwapitia wanachama wake na kuwahimiza wale ambao wana sifa, lakini hadi sasa hawana ili waweze kuvipata.Mwenyejkiti wa Baraza hiyo ya Msumbiji, Mohammed Umbaya amemweleza Katibu Mkuu kuwa wanachama kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar hufika katika Baraza hiyo kwa ajili ya kupata taarifa za chama, pamoja na matukio yanayotokea nchini na Duniani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.