Na Mariam Kamgisha, Ulanga
WANANCHI wa jimbo la
Ulanga Magharibi, wilayani Ulanga mkoani Morogoro, wamemuomba Rais Jakaya
Kikwete, kutimiza ahadi yake aliyowapa
wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2010 za kuwapatia wilaya mpya.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara kwenye vijiji na makao makuu ya
tarafa nne za wilaya hiyo za Lupiro, Mtimbira, Malinyi na Ngoheranga, baadhi ya
wananchi hao,walidai wanashangazwa na ugumu unaojitokeza katika upatikanaji wa
wilaya mpya, wakati Rais Kikwete aliwaahidi wakati wa kampeni.
Kwa nyakati tofauti
baadhi ya wananchi hao walibainisha umuhimu wa wilaya mpya ili kusogeza huduma
za kijamii na za kiuchumi kwa karibu, huku wale wa Minepa, wakimtuhumu diwani
wao Athumani Kapati kuwashawishi wananchi kukubali Lupiro iende Ulanga mashariki,
huku diwani huyo akikanusha madai hayo.
Wananchi hao walidai
wana hofu kuwa mchakato huo umeanza kuingiliwa na mmoja wa viongozi wa juu serikalini,
ambaye anatoka Ulanga Mashariki, (Celina Kombani, Mbunge wa Ulanga Mashariki na
Waziri wa nchi ofisi ya Raisi, Utumishi) ambaye anafanya kampeni za kukwamisha
mchakato huo.
Aidha aliwasema
Waziri huyo anawashawishi wataalamu wa wilaya na mkoa wakubali tarafa ya Lupiro
ihamishiwe Ulanga mashariki kwa maslahi yake binafsi.
Walidai kiongozi
huyo huwaeleza watu wa Malinyi kuwa iwapo Lupiro itaaondoka katika jimbo hilo,
makao makuu yatakuwa Malinyi na vivyo hivyo akiwaeleza wananchi wa Mtimbira
kuwa wakifikia maamuzi hayo, basi makao makuu ya wilaya yatakuwa katika eneo
hilo, mambo ambayo yanalenga kuwachanganya wananchi.
Akizungumza na
wananchi hao,Mbunge wa jimbo la Ulanga Magharibi, Dk. Haji Mponda, aliwataka
kuwa na subira wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kupata wilaya mpya, na
kukiri iwapo Lupiro itaondolewa Ulanga magharibi, kuna hatari ya jimbo hilo
kukosa wilaya, kwani jimbo hilo lina tarafa nne tu.
No comments:
Post a Comment