Na Fatina
Mathias, Dodoma
KAMATI kuu ya
Baraza la Watoto Tanzania, imewataka baba na mama zao wanaounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKAWA) kurudi bungeni ili kukamilisha kazi waliyoianza kwani ni
pigo kubwa kwa watoto.
Tamko hilo
lilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya baraza hilo,Ummy Jamaly, wakati
akitoa tamko la baraza hilo
mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Alisema watoto
hawaridhishwi na mwenendo mzima wa bunge la katiba hasa kwa baadhi ya wabunge kususia mchakato huo na
kuhatarisha ukamilishaji wa katiba ambayo ni muhimu kwa mustakabali wa watoto nchini.
“Kwa sababu
yoyote ile kutokamilika kwa katiba ni pigo kubwa kwa watoto si tu kwa kuwa ni
kundi kubwa la watu nchini bali pia ni muda mrefu haki za watoto hazikupata
nafasi ya kutosha katika michakato mbalimbali ya jamii,” alisema.
“Tunatoa wito
kwa baba na mama zetu wa kundi la UKAWA kurudi bungeni mara moja ili kukamilsha
kazi hii muhimu kwa ajili ya taifa letu,” alisema.
Alisema katika
kuhakikisha haki za watoto zinaingizwa
katika rasimu ya katiba mpya, wamefanya mikutano mingi ya ushawishi na viongozi
mbali mbali wakiwemo wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Pia baraza hilo ilimeomba haki za watoto zibaki katika katiba mpya kama ilivyotajwa kwenye rasimu ya pili ya katiba ibara ya
43.
Walitoa wito
kwa wabunge wa bunge la katiba kuyapa kipaumbele mapendekezo ya watoto ambayo
yalikuwa muhimu yawemo katika katiba mpya.
Aliyataja
mapendekezo hayo ni malengo ya taifa, tafsiri ya mtoto, haki ya kupata elimu,
haki ya kupewa jina, uraia, mtoto kutopewa adhabu kali ikiwemo viboko na
mabaraza ya watoto kutambulika kikatiba.
Pia haki ya
mtoto kupata huduma ya afya, wajibu wa mtoto, haki za wanawake,uwakilishi wa
watoto bungeni, tume ya taifa ya haki za watoto, kuwepo na Wizara ya watoto tu
na masuala ya muungano.
Kwa upande
wake, Waziri Simba alisema wajumbe wa UKAWA wanaombwa kurudi bungeni ili
wakubaliane na kupiga kura kama wakiridhia.
Alisema rasimu
ya Jaji Joseph Warioba iliweka vipengele vyenye maslahi kwa watoto na sasa
vinajadiliwa kwenye kamati na katiba itabeba mambo yenye maslahi kwao.
“Tumekubaliana
mtoto ni yule aliye na umri chini ya miaka 18 na suala la watoto kuchapwa
viboko litawekwa kwenye sheria,” alisema.
Alisema sasa
serikali haina uwezo wa kuweka wizara itakayoshughulikia masuala ya watoto pekee.
No comments:
Post a Comment