Na Maryam Talib, Pemba
ONGEZEKO la gharama za
uendeshaji ikiwa ni pamoja na bei ya mafuta, imetajwa ndio sababu ya kuondolewa
ruzuku ya ukulima wa matrekta kwa wakulima wa mpunga kisiwani hapa.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi, Ofisa Mkuu Kilimo Pemba, Amour Juma Mohammed, alisema awali
serikali ilikuwa ikiwalimia wakulima kwa bei ya shilingi 16,000 kwa ekari moja,
huku ikifidia baadhi ya gharama.
Lakini kutokana na ongezeko la
gharama za uendeshaji wa matrekta zinazojumuisha vipuri na mafuta, ilisababisha
wasimamizi wa kilimo cha matrekta kurejesha gharama katika uhalisia wake.
Alisema iwapo wangeendelea
kubakisha bei hiyo, wasingemudu kuwafikia wakulima wote waliokuwa wakihitaji
huduma hiyo kwa vile gharama zilikuwa kubwa kuliko uwezo wa kuendesha.
Alisema hali hiyo ndio iliyosababisha
bei ya kulima kupanda kutoka shilingi 16,000 hadi shilingi 32,000 na kwamba
maamuzi hayo yalifikiwa kwa makaubaliano na maofisa wa kilimo
wanaoshughulika
na ukulima wa matrekta.
“Kwa miaka mitatu kuanzia 2011 serikali
ilitoa ruzuku ya punguzo la ukulima, kwa bahati msimu wa mwaka 2014 ruzuku ile
ya mfuta ilikuwa imemalizika na sisi kama viongozi tukaona tuongeze bei kidogo
ili wakulima waweze kulimiwa,”alisema.
Baadhi ya mabwana shamba na maofisa
wa kilimo wilaya za Pemba, walisema ruzuku ya mafuta imekuwa kikwazo wakati
msimu wa kilimo unaofika.
Hamad Ali Hassan alisema
wakulima wamekuwa hawajui matatizo hayo, bali wanachokifahamu wao ni kulimiwa na
kwamba inaweka mkazo zaidi kwenye kilimo.
Mratibu wa pembejeo wilaya ya
Wete, Hamad Ali Hassan, alisema mafuta wanayopewa ni tofauti na Unguja, kwani
Pemba maeneo mengi ni mabonde wakati Unguja maeneo mengi ni tambarare.
Nassor Hamad Khamis, ambaye ni bwana
shamba wilaya ya Wete, alisema licha ya mafuta, usumbufu mwengine ni
upatikanaji wa matrekta, kwani yaliyopo hayatoshi kutokana na idadi ya wakulima
wanaohitaji huduma hiyo.
Alisema wakati mwengine matrekta
huharibika hali inayorudisha nyuma na kuvunja matumaini ya wakulima msimu
unapofika.
Alisema serikali inapaswa
kutengeneza matrekta hayo ili kuondoa usumbufu kwani hali ya ulimaji kwa
kutumia jembe la mkono umekuwa tatizo.
Naye Nassor Mwalim Kai
bwanashamba, alisema serikali inapaswa kuweka kipaumbele katika kutoa mafuta
kwa wakati.
Hamad Omar Mohamed, mkuu wa
kitengo cha Ufundi na Uhifadhi wa zana za kilimo Pemba, alisema kitengo chake
kinakabiliwa na uchakavu wa matrekta na kusababisha kufanya kazi kwa kiwango
cha chini.
Alithibitisha kwamba mtrekta
mapya yalikuja katikati ya msimu wa mwaka huu na kusema yanafanya kazi lakini
nguvu zake ni ndogo tofauti na makongwe yaliyopo.
Alisema uwezo wa trekta kwa
siku linaweza kulima ekari nane mpaka 12 lakini kutokana na uwezo mdogo pamoja
na ugumu wa ardhi hulima ekari 5 hadi sita.
Ali Mohamed Omar Mkuu wa Idara
ya Uhakika wa Chakula na Lishe Pemba, alisema idara hiyo ipo na imeanzishwa kwa
sheria namba 5 ya mwaka 2011 na tayari imeshateua baadhi ya wafanyakazi na
kutolewa miongozo.
Amour Juma Mohammed, Ofisa Mkuu
Kilimo Pemba, alisema msimu uliopita serikali haikuongeza mafuta katika bajeti
yao, huku wilaya za Micheweni, Wete na Chake Cheke kwa msimu uliopita zimepata
mavuno madogo.
Mratibu wa Pembejeo za Kilimo wilaya
ya Chake Chake, Mohammed Khamis Haji, aliiomba serikali kununua majembe mapya
ya kulimia kuliko kununua vipuri vya kutengeneza.
No comments:
Post a Comment