Habari za Punde

Ligi daraja la kwanza Kimbunga na Muungano Rangers yatoka sare bila ya kufungana


TIMU ya soka ya Kimbunga imeshindwa kukitambia kiwanja chake cha nyumbani kwa kulazimishwa sare isiyokuwa na mabao katika mchezo wa ligi daraja la kwanza Taifa uliochezwa uwanja wa Tazari.
 
Kimbunga ambayo ilikuwa mwenyeji wa mchezo huo ilishuka uwanjani hapo kuumana na timu ya Muungano Rangers ambayo imepanda daraja msimu huu.
 
Katika mchezo huo timu zote zilionekana kucheza kwa kukamiana jambo lililopelekea kuleta ushindani wa hali ya juu na kutoa burudani tosha machoni mwa mashabiki waliohudhuria mchezo huo.
 
Miamba hiyo iliyokuwa ikiendelea kushambuliana kwa zamu ililazimika kumaliza dakika 90 ikiwa si Kimbunga wala Muungano alieweza kuuona mlango wa mwenziwe na miamba hiyo kugaiana pointi moja kila mmoja.
 
Huko katika uwanja wa Dunga pia mwenyeji wa uwanja huo timu ya Idumu nayo ikalazimishwa sare ya bila ya mabao na timu ya Bweleo.
 
Ligi hiyo itarajiwa kuendelea tena Septemba 26 mwaka huu, kwa michezo mitatu ambapo katika uwanja wa Mao Uhamiaji itakuwa uso kwa uso na Kijichi, wakati wa saa 8:00 na saa 10:00 Black Sailor atapambana na BZL, ambapo katika uwanja wa Mwanakombo Coast Stars atacheza na Mahonda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.